Na Mathias Canal, Kiteto-Manyara
Daraja korofi katika barabara inayounganisha Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara na wilaya za Mvomero na Gairo Mkoa wa Morogoro, Kongwa na Kibagwa mkoani Dodoma limepatiwa ufumbuzi wa kudumu na serikali baada ya ujenzi kukamilika.
Daraja hilo lililopewa jina la Mama Samia Lekaita Kiseru katika Kijiji na Kata ya Sunya Wilayani Kiteto limekamilika baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya ujenzi.
Akizungumza leo tarehe 21 Septemba 2023 kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kijiji cha Chang'ombe, Olgira, na Mbikasi akiwa katika ziara ya Jimbo ya siku tatu kuanzia tarehe 21/23 Septemba 2023 Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mhe Edward Ole Lekaita amempongeza Rais Samia kwa uthubutu wake wa kujenga daraja hilo lililokuwa kikwazo kwa wananchi huku likikusudiwa zaidi kurahisisha usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Amesema kuwa maendeleo yanayofanywa na Rais Samia yanaacha alama kubwa na tunu katika wilaya ya Kiteto na nchi kwa ujumla kwani amejipambanua kuwa kiongozi mwenye kubeba maono ya maendeleo endelevu.
Pia Mbunge Ole Lekaita ameipomgeza serikali kwa kukubali na kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kongwa (Hogoro) – Kibaya – Orkesimet – Oljoro – Arusha pamoja na barabara ya Chemba, Kiteto, Kilindi hadi Handeni mkoani Tanga.
Kadhalika, ameipongeza serikali kwa kurahisisha huduma za upatikanaji wa elimu kwa kujenga shule shikizi ambapo amesema kuwa tayari mchakato umeanza wa kusajili shule hizo zote katika wilaya ya Kiteto ili ziwe shule kamili.
0 Comments