Ticker

6/recent/ticker-posts

MGAMBO JKT, KABUKU LIMEITIKA KILIMO CHA ZAO LA MKONGE,

Dc Wakili Msando akiongea na hadhara pamoja na vijana waliomaliza mafunzo.
Kanali Amos Moro akitoa taarifa ya JKT makao makuu ambapo alimuwakilisha Mkuu wa JKT nchini Brigedia Jenerali Rajabu Mabele.
Kamanda wa kikosi cha 835 Kabuku JKT. Kanali Raymond Mwanry akitoa taarifa ya kikosi hicho kuhusu wahitimu wa mafunzo.
Vijana wa mujibu wakimsikiliza Dc Wakili Msando kabla ya kufunga mafunzo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando akikagua gwaride la vikana wa mujibu wa sheria, kikosi Operesheni ya miaka 60 ya JKT, Mgambo 835, Kabuku JKT.
Shamba la mkonge ambalo linalimwa na kambi hiyo ya Kabuku ikiwa ni moja ya njia ya kujiongezea kipato.
Kanali Mwanry akitoa maelezo kuhusu shamba la mkonge unaolimwa na jeshi hilo.


****************

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

TAASISI za serikali zimetakiwa kushirikiana na Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kikosi namba 835 Mgambo Kabuku iliyoko wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, kwenye suala la kilimo cha zao la Mkonge ili iweze kufanikiwa kwa haraka katika harakati za kukuza zao hilo la kimkakati.


Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi, kambi ya Mgambo, kikosi namba 835, operesheni ya miaka 60 ya JKT, ambapo amewapongeza kwa kujiongezea kipato na uzalishaji wenye tija.


"Na niwaagize wale wote wanaopaswa kushirikiana nanyi, taasisi za serikali waje kwa ukaribu sana ili mipango yenu mliyonayo iweze kufanikiwa kwa haraka, kwahiyo namuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hii na timu yake wafike hapa mkae nao mpange" amesema


"Serikali imeleta vifaa vya kisasa, vikiwemo vya kupimia udongo kwa garama kubwa, hivyo nendeni mkavitumie kuhakikisha kwamba kilimo mnachokifanya kiwe cha kisasa lakini pia kiwe cha mfano, nataka jeshi lenyewe sasa lioneshe kuwa tunaweza kutumia kilimo kwa kuwakwamua wananchi wetu kiuchumi" amesisitiza.


Aidha Wakili Msando amelipongeza jeshi hilo kwa namna lilivyowalea vijana kwani anaamini kwamba wameweza kutambua uzalendo wao kwa nchi yao, lakini pia aliwaasa vijana hao kuwa nidhamu ndiyo kitu pekee muhimu itakayowalea kokote waendako baada ya kupatiwa mafunzo hayo.


Akimuwakili Kamanda mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Rajabu Mabele, Kanali Amos Moro amesema kuwa jeshi limejiridhisha kwamba vijana waliopatiwa mafunzo hayo wamehitimu katika viwango mujibu wa sheria za jeshi hilo kutokana na umahiri wao waliouonesha ikiwemo sanaa.


Kanali Moro amebainisha kwamba katika mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa muda wa majuma 12, sawa na miezi mitatu, wanakikosi wametekeleza kikamilifu majukumu makuu matatu ya JKT ambayo ni malezi ya vijana, uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.


"Mafunzo haya yametolewa kwa muda wa majuma 12 na vijana wamejifunza mafunzo ya darasani kinadharia pamoja na uwanja wa medani, kazi za mikono na uzalishaji mali, lengo likiwa ni kukuza moyo wa kizalendo, kuwafundisha ukakamavu, ujasiri, uwezo wa kutumia muda vizuri na kuwafanya wajitambue kuwa wao pia ni sehemu ya jamii ya Watanzania wanaopaswa kupata mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa" amesema.


Akitoa taarifa, mkuu wa kikosi cha Mgambo JKT Kabuku, Raymond Mwanry amesema vijana hao walianza mafunzo yao rasmi juni 19, 2023 na walifanya ndani ya majuma 12 mfululizo bila kusimama ambapo pia waliweza kujifunza mambo mbalimbali kama ilivyoelekezwa kutoka JKT makao makuu.


"Vijana hawa kwa kipindi chote walichokaa hapa walifundishwa masomo yaliyokusudiwa kwa kufuata mwongozo na silabi ya sheria ya mujibu wa vijana kutoka makao makuu, kupitia mafunzo hayo vilevile vijana hawa sasa wapo timamu wanaelewa nini maana ya ulinzi, wa Taifa lao na ulinzi wao binafsi" amesema.


"Wamejifunza pia uzalendo na nchi yao, utii kwa mamlaka zilizowekwa kisheria, uhodari katika kutekeleza majukumu yao, ushirikiano baina yao kama Watanzania, kiapo walichokiapa leo wameeleweshwa maana yake na ni matumaini yetu kuwa watakiishi kiapo chao kule watakaenda" amebainisha.


Akisoma risala ya kikosi hicho, Salma Mzule ambaye ni muhitimu wa mafunzo amesema katika kipindi chote cha majuma 12 wamekumbana na matatizo mbalimbali pamoja na juhudu za makao makuu ya JKT kuwachimbia visima vitatu vya maji bado kuna tatizo la kukosekana kwa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.


"Kikosi hiki kinapata maji kutoka mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira (HTM) Wilaya ya Korogwe, aidha upatikanaji wa majisafi kutoka mamlaka hiyo yalikuwa ya kuridhisha kidogo lakini hayakuwa safi na salama kwa kunywa, jambo ambalo tulihofu kuhatarisha afya zetu,


"Sisi vijana wa mujibu wa sheria operesheni miaka 60 ya JKT tunapendekeza kwamba (HTM) iboreshe miundombinu yake ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa majisafi na salama katika kikosi hiki" amebainisha Mzule.

Post a Comment

0 Comments