Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS KATIKA MKUTANO WA FFD

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kukabiliana na upungufu wa fedha za maendeleo ili kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) duniani.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akichangia katika mjadala wa viongozi wa ngazi ya juu kuhusu ufadhili wa maendeleo uliyokuwa na dhima ya kutafuta suluhisho la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.

Makamu wa Rais amesema ili kushawishi sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ni vema mataifa yakajielekeza katika kuweka sera rafiki kwa sekta binafsi.

Ameongeza kwamba kupitia ripoti ya hivi karibuni ya Mtazamo wa Kiuchumi wa Afrika (AEO 2023) kuhusu ufadhili mbadala, inabainisha wazi kuwa sekta ya binafsi ni miongoni mwa wadau muhimu katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kwa kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa, Tanzania imefanikiwa kuwa na njia mbalimbali za ufadhili ambazo ni rafiki kwa sekta binafsi ikiwemo kutengeneza ramani ya wawekezaji ya malengo ya maendeleo endelevu.

Ameongeza kwamba katika uboreshaji wa miundombinu, Tanzania imetumia mbinu ya Ufadhili wa Mikataba ya Ujenzi na Ununuzi wa Kihandisi (EPC+F) ili kuongeza ufadhili wa sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri.

Makamu wa Rais ametaja mifano mingine kuwa ni pamoja na utoaji wa hati fungani ya kwanza nchini yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 300 iliotolewa na Benki ya CRDB kwa lengo la kufadhili miradi rafiki ya mazingira ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta za miundombinu, nishati mbadala , viwanda, ujenzi na usambazaji maji.

Vilevile Makamu wa Rais amesema kwamba ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi nchini Tanzania katika kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuinua kipato cha watu, Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa benki za biashara kwa ajili ya kukopesha wakulima kwa riba isiyozidi 9%.

Amesema matokeo ya mpango huo wa ushirikiano yameleta tija ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwenye sekta ya kilimo kuongezeka kutoka asilimia 7.3 katika mwaka ulioshia Julai 2021 hadi asilimia 46.4% Julai mwaka 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa Mjadala wa Viongozi wa Ngazi ya Juu kuhusu ufadhili wa maendeleo uliyokuwa na dhima ya kutafuta suluhisho la kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.

Post a Comment

0 Comments