Ticker

6/recent/ticker-posts

DMDP II MBIONI KUANZA KAZI ZA UJENZI

SERIKALI na Benki ya Dunia wamekubaliana kuanza haraka utekelezaji kazi za ujenzi wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Septemba 26, 2023 kwenye kikao kilichowakutanisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deo Ndejembi, Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. John Motton na Mhandisi Humphrey Kanyenye ambaye ni Mratibu wa Miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Kikao hicho kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo za Wizara zilizoko Dar es Salaam kimelenga kujadili namna bora ya kuanza kazi za ujenzi katika Mradi DMDP II na uhifadhi wa taka ngumu.

Katika kikao hicho viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kuwa kazi ya usanifu yakimifu ikamilike ndani ya muda na mpaka Novemba mwaka huu wakandarasi wawe wamewasilisha kwa ajili ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza kazi za ujenzi ziweze kuanza mara moja.

Pia wamekubaliana na kupitisha maeneo yaliyopendelezwa kwa ajili ya kujengwa madampo ya kisasa katika Mkoa wa Dar es salaam katika Halmashauri za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni.

Viongozi hao pia walikubaliana kuwa ili kuwe na udhibiti madhubuti wa taka ngumu ni vyema ikaanzishwa Wakala utakaosimamia udhibiti wa taka ngumu kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments