Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. RWEZIMULA -UONGOZI BORA WA SHULE UNASAIDIA KUIMARISHA USIMAMIZI WA UFUNDISHAJI NA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA SHULE

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amefunga Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika Elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo jana Septemba 28,2023 iliyofanyika Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa elimu nchini (ADEM), Dkt. Rwezimula amesisitiza kuwa uongozi, usimamizi na uendeshaji wa elimu una mchango mkubwa katika Maendeleo ya shule na elimu kwa ujumla.

Aidha amesema uongozi bora wa shule unasaidia kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, kusimamia rasilimali za shule, utekelezaji wa miradi, kuboresha udhibiti wa shule kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inathimini mchango wenu ADEM katika kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule na elimu kwa ujumla hapa nchini” na kuongeza

“ADEM ina wajibu wa kuisaidia serikali kufikia malengo ya mabadiliko ya elimu kwa kutoa mafunzo na kufanya utafiti ili kuimarisha uongozi , usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini.”

Hata hivyo Dkt. Rwezimula amewataka washiriki wa mafunzo hayo kubadilika kutokana na namna walivyopata mafunzo na kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali.

“Tunatarajia kuona mabadiliko chanya na endelevu katika uendeshaji wa shule. Matokeo ya mafunzo yatapimwa katika utendaji wenu kupitia viashiria vya ufanisi ,kama hakutakuwa na mabadiliko basi utakuwa ni upotevu wa rasilimali fedha na muda” alisisitiza Dkt. Rwezimula

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Alphonce Amuli amesema, mafunzo yaliyotolewa yamelenga kuimarisha utendaji kazi wao na kuwapa uwezo wa kuyamudu majukumu mapya na majukumu waliyonayo awali ambayo walikuwa wanayatekeleza kwa uzoefu na si ufanisi.

Dkt. Amuli ameendelea kwa kusema kuwa, mara baada ya mafunzo hayo kukamilika hatua ya ufuatiliaji na tathimini itafanyika katika shule ambazo wanatoka washiriki hao kupima uzingativu wa walichojifunza na viashiria vya ufanisi na umahiri.

“Tunatarajia kuona mabadiliko baada ya mafunzo kwa yale yote ambayo wamefundishwa huku zoezi la ufuatiliaji likifanyika katika shule ambazo washiriki wa mafunzo wametoka kuona kama kuna mabadiliko yametokea” alisema Dkt.

Akitoa taarifa fupi kuhusu mwenendo wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo huyo Bw.Richard Sungura ameeleza kuwa, mafunzo hayo yanaendeshwa kwa awamu mbili kwa walimu wakuu 608 katika halmshauri zote 9 za Mkoa wa Pwani kuanzia Septemba 26, 2023 hadi Oktoba Mosi, 2023

Sungura ameendelea kwa kusema kuwa, awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yameanza Septemba 26, 2023 hadi Septemba 28, 2023 kwa washiriki kutoka halmshauri za Chalinze, Bagamoyo, Kibaha mji, Kibaha vijijini, Kibiti na Rufiji ambapo jumla ya walimu wakuu 365 wamshiriki mafunzo hayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula akisisitiza jambo wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani Septemba 28, 2023
Kaimu Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt Samia Alphonce Amuli akiongea wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani.
Mratibu wa Mafunzo kutoka ADEM Richard Sungura, akitoa taarifa ya mwenendo wa mafunzo kwa mgeni rasmi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani akisoma ushahiri
Washiriki wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika elimu wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na Utawala Bora katika elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa kutoka ADEM na baadhi ya washiriki mara baada ya kukamilika kwa hafla ya kufunga mafunzo hayo

Post a Comment

0 Comments