Ticker

6/recent/ticker-posts

DC ULANGA AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA


Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst) Rose Teemba (Katikati), Wajumbe wa Baraza, Mawakili wa Serikali na Dkt. Julius Ningu, Mkuu wa wilaya ya Ulanga (wa kwanza kushoto) wakiwa katika kikao cha Baraza la Maadili jijini Dodoma Septemba 5, 2023.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro, Mhe. Dkt. Julius Kenneth Ningu akiwa amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma


Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro, Mhe. Dkt. Julius Kenneth Ningu (59) amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na lugha za vitisho dhidi ya watumishi wa umma alipokuwa katika ziara za ukaguzi wa miradi mbalimbali.

Akiwasilisha malalamiko hayo mbele ya Baraza Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Emma Gelani, ameliambia Baraza la Maadili kuwa Dkt. Ningu alifanya vitendo hivyo kinyume na kifungu cha 6 (1)(a) na 6(1)(b)(i) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma akiwa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma kabla ya kuhamishiwa wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro.

“Dkt. Ningu wakati akitekeleza majukumu yake amekuwa akiwakamata na kuwaweka mahabusu watumishi wa umma na wananchi kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.”

Kwa mujibu wa Wakili huyo, kushindwa kutimiza wajibu huo wa kisheria ni ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Wakili Gelani alisema, “Mhe. Mwenyekiti, kitendo hiki ni kinyume na maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia barua yake ya tarehe 1/4/2019 kwenda kwa wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhusu matumizi sahihi ya Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inayotoa utaratibu wa kumuweka mtu mahabusu kwa muda wa saa 48.”

Kwa mujibu wa Wakili huyo Mkuu wa Serikali, maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yanamtaka Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa wilaya kutoa maelezo kwa njia ya maandishi kwa jeshi la polisi kabla au muda mfupi baada ya kuamulu mtu kuwekwa ndani kutoa sababu za msingi za kumuweka mahabusu mtuhumiwa.

“Dkt. Ningu hakutoa maelezo yoyote kwa jeshi la polisi kuhusiana na kukamatwa kwa watumishi wa halmashauri na mafundi waliokuwa wakitekeleza mradi ya UVIKO 19 katika wilaya ya Namtumbo kinyume na maelekezo ya Sheria,” alieleza.

Katika shauri hilo Na.1 la mwaka 2023, upande wa Mlalamikaji ulileta mashahidi watatu.

Bw. Mario Fabian Mwageni, Afisa Mtendaji kata ya Rwinga, wilaya ya Namtumbo, Mkoani Ruvuma aliyekuwa shahidi upande wa mlalamikaji, ameliambia Baraza kuwa mnamo tarehe 22/11/2021 Mkuu wa wilaya alipotembelea Kata yake kukagua shughuli za maendeleo alisema, “wewe na mkuu wa shule ya Rwinga lazima niwaweke ndani ili nionyeshe mfano kwa watumishi wengine kwasababu mnakwamisha shughuli za ujenzi wa madarasa.”

Kwa mujibu wa Mtendaji huyo wa Kata, Mkuu wa wilaya “aliamuru tuingie kwenye gari hadi Namtumbo. Tulipofika Namtumbo, alisema DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) peleka watu hawa ndani mpaka nitakapoeleza vinginevyo.”

“Tuliwekwa mahabusu tangu saa 7:00 mchana hadi saa 3:00 usiku na tukatolewa bila kuambiwa kosa letu na hakuna chochote kilichoendelea,” alieleza.

Kwa upande wake OCD wa wilaya ya Namtumbo Bw. William Abel Mwamafupa amekili mbele ya Baraza kuwaweka mahabusu watuhumiwa kwa amri ya Mkuu wa wilaya bila maelezo.

“Mkuu wa wilaya anatakiwa kuniandikia barua anapotoa amri ya kuwaweka watu mahabusu, lakini tulipokuwa tukienda kukagua miradi ya maendeleo Mkuu wa wilaya alikuwa anaamuru wahusika wa miradi iliyokuwa inasuasua wakamatwe na kuwekwa ndani bila maelezo.”

Alipopewa nafasi ya kujitetea, Dkt. Ningu alikana mashitaka hayo na kusema alifanya hivyo kwa kushauriwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya.

Utetezi wa pande zote mbili umekamilika.

Kikao cha Baraza kimeketi chini ya mwenyekiti Mhe. Jaji (mst.)Rose Teemba na wajumbe wawili ambao ni Bw. Peter Ilomo na Bi. Suzan Mlawi.

Mwenyekiti wa Baraza Mhe. Teemba amesema, “Baraza litakaa litafanya kinachopaswa kufanyika kwa mujibu wa sheria.”

Baraza hilo linafanya kikao chake cha siku mbili jijini Dodoma kuanzia tarehe 5 Septemba, 2023 chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Jaji (Mst.) Rose Teemba akisaidiana na Wajumbe wa Baraza Bw. Peter Ilomo na Bi. Suzan Mlawi.

Post a Comment

0 Comments