Muonekano wa sehemu ya Reli ya Kisasa (SGR) ambayo imeshakamilika.
****
BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) baada ya kutembelea na kukagua vipande vitano vya mradi huo.
Vipande hivyo ni cha Dar es Salaam - Morogoro ambacho kimefikia asilimia 98.8, Morogoro - Makutupora asilimia 94, Makutupora - Tabora asilimia 12, Tabora - Isaka asilimia tano na Mwanza - Isaka asilimia 39.
Akizungumza leo Septemba 19, 2023 jijini Mwanza baada ya kukagua ujenzi wa kituo kikuu cha reli ya kisasa Mwanza, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TRC, Ally Karavina amesema bodi hiyo ambayo ni mpya imetembelea miradi hiyo kujionea kinachoendelea ambapo wameridhishwa na walichokiona na wana matumaini makubwa itakamilika kwa wakati na kuleta faida kwa watanzania.
"Kazi iko vizuri wakandarasi wanafanya vizuri tumeridhika na tulichokiona. Ni mradi wa kimkakati wenye faida kwa nchi na utabadilisha uchumi wa taifa kuwa wa kati wa juu," amesema Karavina
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Amina Lumuli amesema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kama inavyotakiwa ili ikamilike kwa wakati na Watanzania wafurahie huduma nzuri, huku akisisitiza kuwa TRC imejipanga kuhakikisha uendeshaji wa reli hiyo unakuwa mzuri kulingana na hadhi ya mradi.
"Tuko kwenye ziara na bodi mpya ya wakurugenzi ili wapate uelewa wa kinachoendelea wajue wapi wataanzia lengo ni kuhakikisha miradi tunaisimamia kama inavyotakiwa,"
"Utengenezaji wa mabehewa unaendelea vizuri tulishapokea mabehewa 14 tunatarajia kupokea mengine mapya 15 na mabehewa yote yatakuja, kichwa cha kwanza cha treni tunatarajia kukipokea Novemba, mwaka huu," amesema Amina.
Naye, Meneja Mradi Msaidizi wa kipande cha tano (Mwanza -Isaka), Moga Kulwa amesema wanaendelea na usanifu ambao umefikia asilimia 80 na ujenzi ambao upo asilimia 39 pamoja na utwaaji wa ardhi, ambapo kituo (station) cha Mwanza ambacho ndiyo kitakuwa kikubwa kwenye kipande hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 961 kwa wakati mmoja.
"Tunategemea mradi utakamilika kwa muda katika ubora unaohitajika ili kutoa huduma kwa ubora, mradi huu utakuwa na faida kwa abiria na bidhaa ambao watasafiri kwa haraka (saa nane), reli itaweza kubeba mizigo mkubwa kwa wakati mmoja, usafiri wa bei nafuu na usalama wa hali ya juu," amesema Kulwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) Ally Karavina (mwenye miwani) akipokea maelezo kuhusu ujenzi wa reli hiyo kipande cha tano (Mwanza-Isaka) chenye urefu wa Kilometa 341 kutoka kwa mmoja wa wahandisi katika mradi huo. Mradi huo umefika asilimia 39.
0 Comments