Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MABULA ATAHADHARISHA WANAOTUMIA WIZARA KAMA REJEA KUFANYA UHALIFU

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa tahadhari kwa wale wanaotumia wizara yake kama rejea kufanya uhalifu na kujipatia mali au fedha isivyo halali.

Waziri Mabula amesema mtu yoyote akihisi kuna udanganyifu ndani na nje ya Wizara ya Ardhi atoe taarifa mapema ili kukomesha uhalifu huo.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo leo tarehe 14 Agosti 2023 mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma kufuatia wizara yake kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa familia ya marehemu Zuberi Mzee Mwinyimvua inayodai kwamba wizara yake haitaki kuondoa Hati ya kuwekesha (Notice of Deposit) iliyosajiliwa katika daftari la Msajili wa Hati kuhusu kiwanja Na 895 kilichopo eneo la viwanda mbezi mkoani Dar es Salaam iliyiosajiliwa ili kutoa kinga ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kiwanja hicho kinamilikiwa na Mwinyimvua ambaye kwa sasa ni marehemu.

Akifafanua zaidi, alisema awali mmiliki wa kiwanja hicho aliingia mkataba wa uwekezaji na Velence Simon Matunda na Badi Nkya wanaotambulika kama wawekezaji.

Uwekezaji huo ulikuwa ni kujenga maduka 40 ambapo kati ya hayo maduka 33 yangesimamiwa na wawekezaji kwa kipindi cha miaka 15 na baada ya hapo wangekabidhi maduka hayo 15 kwa mmiliki ambapo katika kipindi hicho cha miaka 15 wawekezaji wangekusanya kodi ya pango.

Kwa mujibu wa mkataba, mmiliki alipewa kiasi cha shilingi 90,000,000 kwa ajili ya kulipa madeni ikiwemo kodi ya pango la ardhi la kiwanja hicho.

Waziri Mabula alisema suala la mgogoro huo limekuwa likishughulikiwa kiutawala kupitia wizara ya ardhi kwa zaidi ya miaka 8 kuhakikisha kwamba wawekezaji wanalipwa fedha hizo kama mahakama ilivyoamuru ili hatimaye msajili wa hati aondoe hati ya kuwekesha katika daftari la msajili na kukabidhi hati husika.

Kwa mujibu wa waziri Mabula, mpaka sasa suluhu ya mgogoro huo haijapatiakana kutokana na pande mbili za mgogogoro yaani msimamizi wa mirathi na wawekezaji kutotekeleza yale waliyokubaliana hususan upande wa uwekezaji.

Kimsingi mgogoro huo unatokana na ukiukwaji wa makubaliano baina ya mmilikina wawekezaji ambapo pia mahakama ilishatoa maamuzi. Wizara inatimiza wajibu wake kiutawala katika kutatua mgogoro pamoja na kuwa suala hilo linahusu mkataba wa uwekezaji na siyo umiliki wa ardhi.

Waziri Mabula alisema kwa kuwa mgogorio huo ni wa muda mrefu na wahusika wanaihusisha wizara ambayo si sehemu ya makubaliano na hivyo kuharibu taswira ya wizara ameelekeza pande zote za mgogoro kuheshimu na kutekeleza hukumu ya mahakama sambamba na pande hizo kutekeleza yale wanayokubaliana katika vikao vya usuluhusshi .

Pia amemuelekeza katibu Mkuu wizara ya ardhi kushirikiana na vyombo vya dola kuingilia kati suala hilo kwa kuwa una sura ya kijinai na utapeli ndani yake.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgogoro wa kiwanja kilichopo eneo la Viwanda Mbezi jijini Dar es Salaam tarehe 14 Agosti 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgogoro wa kiwanja kilichopo eneo la Viwanda Mbezi jijini Dar es Salaam Agosti 14, 2023.

Post a Comment

0 Comments