Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO: TUMWEKEZA MAZINGIRA WEZESHI KWA SMZ KUHAMISHIA SHUGHULI ZA SERIKALI DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahakikishia Wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira wezeshi ya ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Makao Makuu ya Serikali Dodoma.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo lililokabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kujenga Ofisi zake katika eneo la Mahoma jijini Dodoma tarehe 21 Agosti, 2023, Waziri Jafo amesema mwitikio wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutenga eneo la ujenzi wa ofisi Dodoma ni moja ya kielelezo cha dhamira ya dhati ya ushirikiano uliopo baina ya Viongozi na Watendaji wa Serikali zote mbili.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema ili kurahisisha zoezi la ujenzi wa Ofisi hizo za SMZ Jijini Dodoma, Serikali ya Awamu ya Sita imeimarisha miundombinu ndani ya eneo hilo ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za umeme, mitandao ya huduma za mawasiliano huduma ambapo pia baadhi ya balozi na mashirika ya kimataifa yamepatia maeneo katika Mji wa Serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi zao.

“Eneo hilo lina mtandao wa barabara takribani kilomita 52.8, na pia ni moja ya maeneo machache yaliyopo nchini yenye miundombinu imara…Hii ni awamu ya kwanza tunatarajia pia na awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu katika mji wa Serikali” amesema Dkt. Jafo.

Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha itaendeleza maono ya kuasisiwa kwa Muungano kupitia waasisi wake Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuhakikisha wananchi wa pande zote za Muungano wananufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza hatua inayolenga kuharakikisha kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma alimshukuru Waziri Jafo na kueleza kufurahishwa kwake na ukubwa wa eneo hilo iliyopatiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Taasisi zake mbalimbali na kueleza taratibu za ujenzi katika eneo hilo tayari zinaendelea.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Khalid Bakar Amran alimueleza Waziri Hamza kuwa eneo hilo lina ukubwa wa Hekta 33 na SMZ ilipatiwa eneo hilo kama ilivyopeleka maombi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuhamishia Makao Makuu ya Shughuli za Serikali Mkoani Dodoma uamuzi uliokwenda sambamba na kuzingatia wazo la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilolitoa mwanzoni mwa miaka ya 60.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma (kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara ya ya wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za SMZ wa Baraza la Wawakilishi waliotembelea eneo la mradi wa ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Eneo la Mahoma Makulu, Mkoani Dodoma jana Jumatatu (Agosti 21, 2023). Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis katikati akiteta jambo na Mkurugenzi Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Khalid Bakar Amran wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za SMZ wa Baraza la Wawakilishi waliotembelea eneo la mradi wa ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Eneo la Mahoma Makulu, Mkoani Dodoma jana Jumatatu (Agosti 21, 2023).

Wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za SMZ wa Baraza la Wawakilishi wakipokelewa na wenyeji wao Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Khamis Hamza Khamis mara baada ya kuwasili wakati wa ziara yao ya kutembelea Ofisi za Makamu wa Rais zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma jana Jumatatu (Agosti 21, 2023)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (katikati) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za SMZ wa Baraza la Wawakilishi mara baada ya kumalizika kwa kikao baina yao katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma tarehe 21 Agosti, 2023.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

Post a Comment

0 Comments