Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAOINGIZA BIDHAA KIMAGENDO TANGA, TRA YAOMBA USHIRIKIANO


****************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.




WAFANYABIASHARA Mkoa wa Tanga wameaswa kutowafumbia macho badala yake kuwafichua baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kimagendo mkoani humo kwani ni kinyume cha sheria lakini pia huathiri pato la Taifa.


Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Tanga Thomas Masese ametoa wito huo kwenye kikao chake na wafanyabiashara hao jijini humo na kusema kumekuwa na baadhi ya wanaoingiza mizigo kinyemela hali inayosababisha kutolipa kodi na kuisababishia serikali hasara kwakuwa fedha nyingi zinapotea.


"Nitoe wito kwa viongozi wa vyama vya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na TRA kufichua na kukemea udanganyifu unaofanywa na baadhi ya waingizaji wa mizigo nchini ili kunusuru mapato ya serikali, afya za wananchi wetu pia kwa usalama wa nchi yetu" amesema.


"Mkoa wetu bado una tatizo kubwa la magendo ambayo husababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali, mathalani kwa kipindi cha kuanzia mwezi januari 2023, TRA imekomboa kiasi cha zaidi ya sh milioni 130 ikiwa ni kodi pamoja na adhabu kwa mizigo ya magendo iliyokamatwa" amefafanua.


Aidha meneja Maseje ameongelea kuhusu suala la matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD), kwamba hurahisisha utunzaji wa kumbukumbu unapoelekea kodi sahihi kukusanywa kwa wafanyabiashara.


"Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao kwa njia tofauti tofauti hukwepa kutumia EFD, mfano halisi ni kuporomoka kwa matumizi yake ambao ulichagizwa na mgomo wa matumizi ambao ulichagizwa na mgomo wa wafanyabiashara wa mwezi mei, 2023 uliosababisha ufuatiliaji wa matumizi ya EFD kusitishwa kwa muda" ameeleza.


Hata hivyo Maseje amesema kuwa jabeti ya mwaka 2023/24 ni sh trilioni 44.36, na TRA imepewa jukumu la kukusanya sh trilioni 26.73 ambalo ni ongezeko la sh trilioni 3.08 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2022/23.


"Kwa Mkoa wetu wa Tanga mwaka huu tumepewa lengo la kukusanya sh bilioni 215.04, mwaka 2022/23 lengo lilikuwa ni sh milioni 232.64 na tulikusanya sh milioni 214.39 sawa na asilimia 92,


"Mafanikio haya ni yetu sote ninyi wafanyabiashara kwani kodi mnayolipa na kuiusanywa na TRA hutumika katika ujenzi wa Taifa letu kwa kuboresha huduma za kijamii na kujenga miundombinu kwa ustawi wa wananchi wote" amesema.


Maseje pia amewaomba wafanyabiashara kutoa ushirikiano katika ukusanyaji wa kodi lakini pia TRA imepanga kuendelea kutoa elimu kupitia njia mbalimbali ikiwemo ya kukutana na wadau mara kwa mara ili kuweza kutatua kero mbalimbali zinazoweza kuathiri makusanyo ya kodi.


Vilevile amewakumbusha viongozi na washauri wa kodi juu ya ukomo wa ulipaji wa kodi ya mapato awamu ya tatu na kuwataka kuwafikia wanachama na wateja wao kuhusu suala hilo ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kuhamasika na kulipa kodi kabla ya septemba 30, 2023.


"Aidha kwa wale wenye madeni mbalimbali ya kodi kwa kipindi cha nyuma, nawakumbusha kulipa au kuja ofisi zetu za TRA na kuingia mikataba ya malipo ya madeni yao hayo kwa unafuu" amefafanua Maseje.

Post a Comment

0 Comments