Ticker

6/recent/ticker-posts

TGNP YAWAKUTANISHA WANAHABARI NA VIONGOZI WA VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA


*************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imewakutanisha Waandishi wa habari na viongozi wa Vituo vya Taarifa na Maarifa kwaajili ya kujadili ni namna gani wanaweza kushirikiana katika kuhakikisha wanatokomeza masuala ya Ukatili wa kijinsia pamoja na upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwenye maeneo wanayoishi.

Akizungumza katika kikao hicho Jana Agosti 17,2023 Jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Bi. Jachrine Mtesha amesema mpaka sasa kuna vituo vya Taarifa na Maarifa 75 katika mikoa 15 hapa nchini na bado wanaamini vitaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Aidha amesema umuhimu wa vituo hivyo ni kujenga uwezo wa jamii kupata habari,taarifa na kuendesha/kushiriki mijadala mbalimbali inayohusu utu na usawa wa kijinsia na haki za kijamii kazi ambayo vituo hivyo imeendelea kuifanya kwa ufanisi mkubwa.

Nae Mwenyekiti wa Kituo cha Majoe Bi. Tabu Ally amebainisha changamoto aliyowahi kukumbana nayo ya kukamatwa na baadhi ya Viongozi wa ngazi ya Serikali ya mtaa na kuwekwa Kituo cha Polisi kwa siku kadhaa kutokana na viongozi hao kutoelewa na kuhisi analengo la kuwa juu yao.

Ameongeza kuwa baada ya kadhia hiyo kupita hivi sasa wamewaelewesha viongozi hao na wanafanyakazi kwa ukaribu zaidi katika kupigania maendeleo ya jamii zao hasa katika maeneo ambayo yanawazunguka.

Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa, Kivule Bi Zahara Mohamed Mzee amesema awali walipokuwa wanaanza kazi katika jamii walikumbana na changamoto ya Viongozi wengi kutokuwa na Imani nao na kudhania kuwa Wanamalengo ya kuwapindua katika nafasi zao katika siku za usoni hivyo kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwao.

Aidha Bi Zahara ameyataja mafanikio waliyoyapata ikiwa ni pamoja na kujenga Ushirikiano wa karibu na viongozi hao kuanzia ngazi ya Serikali ya mtaa na hadi Polisi,pia wamefanikiwa kuianisha vipaumbele mbalimbali vya jamii vilivyosaidia kujengwa kwa zahanati,shule,matundu ya vyoo,barabara,ununuzi wa vifaa na ukamilishaji wa Ujenzi wa chumba cha upasuaji katika hospital ya Wilaya Ilala kivule.

Mwaka 2010 mtandao wa kijinsia hapa nchini TGNP ulianzisha vituo vya taarifa na maarifa kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwa kuhakikisha changamoto hizo zinafika katika mamlaka husika na kupatiwa ufumbuzi

Tangu wakati huo yapata Miaka 13 vituo hivyo vimeleta mafanikio makubwa kwa jamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuipa jamii hususan wanawake sauti ya kusemea vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia na hata kupeleka maendeleo katika maeneo yaliyo nyuma katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara,shule na hata upatikanaji wa huduma za afya

Huku mtandao huo ukiwa unatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwezi oktoba mnamo mwaka 1993 ni wazi vituo vya taarifa na maarifa ni moja ya mambo ambayo unaweza kujivunia nayo.

Post a Comment

0 Comments