Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kusimamia wakandarasi wanaojenga vivuko kuhakikisha wanajenga vivuko vyenye ubora na tija katika utoaji huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, Bungeni jijini Dodoma, wakati Kamati hiyo ilipokuwa ikipokea taarifa ya Wakala huo kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini.
“Hakikisheni mnafuatilia kwa karibu wakandarasi mnaowapa kazi za ujenzi wa vivuko, tunataka tuone wananchi wanafaidika na vivuko hivi ambavyo serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika ununuzi na ujenzi wake”, amesema Mhe. Kakoso.
Aidha, Kamati pia imeutaka Wakala huo kuhakikisha kuwa inajiendesha kibiashara ili kuweza kuendana na soko la ushindani ndani na nje ya nchi katika kuboresha huduma zake kwa washitiri wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti huyo, pia ameuagiza Wakala huo kuajiri wataalamu wa kutosha sambamba na kuwapatia mafunzo wataalamu walionao lengo likiwa ni kuwaweza wataalamu hao kusaidia na kuongeza nguvu katika ufanisi wa Wakala huo ili kufikia malengo waliojiwekea.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, amesema katika mwaka wa fedha 2023/24 Wakala umepanga kutekeleza miradi mipya 7 ya ujenzi wa miundombinu mipya ya vivuko, vitakavyotoa huduma katika maeneo ya Kisorya-Rugezi, Bwiro- Bukondo, Mafia – Nyamisati, Ijinga – Kahangara, Nyakariri- Kome na Buyangu- Mbalika pamoja na vivuko vidogo viwili (sea tax), vitakavyotumika katika kituo cha Magogoni – Kigamboni.
Naibu Waziri Kasekenya amefafanua kuwa Wakala pia umepanga kukamilisha ukarabati wa vivuko mbalimbali ikiwemo Kivuko cha MV Kazi, MV Misungwi, MV Musoma, MV Tanga na MV TEMESA na kuendelea na kazi za ukarabati wa vivuko 10.
“Kazi za ukarabati wa vivuko zitakazoendelea katika mwaka huu wa fedha 2023/24 zitahusisha vivuko vya MV Kilombero II, MV Kitunda, MV Ruhuhu, MV Old Ruvuvu, MV Sabasaba na MV Kanyabasa”, amesema Kasekenya.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala amesema kuwa Wakala umepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kukamilisha usimikaji na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato katika kivuko cha Magogoni - Kigamboni kwa kutumia kadi ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (haipo pichani) wakati Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ulipokuwa ukiwasilisha taarifa kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini, jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Sekta hiyo akisikiliza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso, akitoa maagizo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini wakati Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ulipokuwa ukiwasilisha taarifa yake, jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala, akisoma taarifa kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (haipo pichani), wakati Kamati hiyo ipokuwa ikipokea Taarifa ya Wakala huo, Bungeni, jijini Dodoma.
Mbunge wa Singida Mashariki, Mheshimiwa Miraji Mtaturu, akitoa maoni yake kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (haipo pichani), ilipokuwa ikipoka taarifa ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bungeni, jijini Dodoma
Baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), wakati Naibu Waziri huyo alipokuwa akiwasilisha taarifa kuhusu uendeshaji wa vivuko nchini, jijini Dodoma.
PICHA NA WUU
0 Comments