Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPANIA KWENDA NA KASI SOKO LA DUNIA ZAO LA KOROSHO,

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akiongea na wadau wa korosho kabla ya kufungua mkutano.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi (CBT), Brigedia Mstaafu, Jenerali Aloyce Mwanjile akitoa taarifa ya Bodi kwa wadau wa mkutano.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akitoa taarifa ya Mkoa kuhusu wakulima wa zao la korosho.

Mwenyekiti wa mkutano wa wadau, Yusuph Mnanila akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.
Wadau wa mkutano wakisikiliza na kufuatilia kwa umakini.

***********************

Wizara ya Kilimo inchini imepanga mkakati wa kuhakikisha inafanya maboresho makubwa katika kilimo cha zao la korosho, ili kuendana na kasi ya soko la Dunia katika biashara ya zao hilo ya kufikisha sh trilioni 21.8 kutoka kiasi cha sh trilioni 17.8 iliyopo.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde ameyasema hayo kwenye mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya korosho mwaka 2023 uliofanyika jijini Tanga jana na kuwashirikisha viongozi, wadau wa kilimo cha zao la korosho, makampuni ya ununuzi kutoka Mikoa yote ambayo inalima zao hilo.


Mavunde amesema kwenye takwimu za soko la Dunia biashara ya zao la korosho kwa msimu uliopita imefanyika biashara ya sh trilioni 17.8 na inakadiriwa ifikapo mwaka 2018 biashara ya korosho itakuwa ni zaidi ya sh trilioni 21.8 Duniani.


"Na hii inatuambia kwamba tukifanya maboresho na uwekezaji mzuri, kuanzia kwenye tafiti na kuwawezesha wakulima kilimo cha tija, iko fursa kubwa sana Duniani kwa zao la korosho na sisi kama serikali tunaiona hii ni fursa na tutakuwa tunaitumia vizuri ili wakulima wetu waweze kunufaika kwa kilimo hiki".


Vilevile Naibu Mavunde amefafanua kwamba kufuatia ufanisi huo serikali bado inaendelea kufanya maboresho makubwa katika tasnia ya korosho.


"Kwanza ni kuongeza bajeti katika kilimo, kwa ajili ya kulipia Pembejeo zinazowasumbua wakulima, ikiwa ni pamoja na ugawaji wa miche bora ya korosho kwa wakulima, na kiasi cha sh bilioni 50 kimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa 2023/24",


"Kuhuisha kazidata za wakulima wa korosho kwa kupima mashamba na kuhesabu idadi ya mokorosho kwa kutumia mfumo wa satelite, kupiga picha wakulima, kuchukua alama za vidole na kumpatia mkulima namba maalumu ya utambulisho ambayo ataitumia kupata pembejeo na pia kuuzia mazoa yake katika msimu ujao" amefafanua.


Pia Mavunde ametoa agizo kwa Bodi ya Korosho kuhusu usajili wa wakulima katika ngazi ya Wilaya, "muwashushe wasajili katika ngazi ya kata ili zoezi letu liweze kwenda kwa haraka na wakulima wetu wasajiliwe wasajiliwe, kwahiyo hili ni jukumu lenu Bodi kuhakikisha mnaongeza wasimamizi".


Hata hivyo ameainisha kwamba sambamba na hilo watapata nafasi ya kujua aina ya wakulima walionao, ukubwa wa mashamba, pembejeo, wanazopokea pamoja na miche waliyonayo ili ziweze kuwasaidia katika takwimu zao katika kuwahudumia wakulima hao.


Mavunde amesema jambo jengine ni kuendelea kuvutia na kuhamasisha uwekezaji mkubwa kwenye ubanguaji na usindikaji wa korosho kwa kutenga eneo la kutosha kwa ajili hiyo katika kijiji cha Maranje, kata ya Mtindiko, halmashauri ya mji Nanyamba mkoani Mtwara, jumla ya ekari 1575 zimetengwa na zitatumika kujenga kongani la viwanda kuanzia mwaka huu wa fedha 2023/24.


"Viwanda hivi vitakuwa na uwezo wa kubangua zaidi ya tani laki 2 kwa mwaka ikiwa ni pamoja na kukamua maganda yote yatakayotokana na korosho hizo, lengo likiwa likiwa kwamba ikifika mwaka 2026/27, korosho zote zibanguliwe hapa nchini na kisha kuuzwa hapa nchini katika masoko ya ndani na nje ya nchi,


"Tafsiri yake ni kwamba kuanzia mwaka 2026 Tanzania hakuna kusafirisha korosho ghafi kwenda nje ya nchi, kupeleka ajira za wananchi wetu nje ya nchi, hio ndio mpango na mkakati wetu kama serikali, na jambo hili linawezekana na likifanyika litatibu vikwazo vingi sana ambavyo vinamkabili mkulima leo" amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments