Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akifungua kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga leo Jumatano Agosti 9,2023
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akifungua kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga leo Jumatano Agosti 9,2023
Wadau wakiwa kwenye kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga
Wadau wakiwa kwenye kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameongoza
kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa wa Shinyanga Halmashauri zote kutilia mkazo siku ya usafi wa mazingira kwa kila Jumamosi ya kila wiki ya mwisho ya mwezi ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza pamoja na vijiji na mitaa yote kufanya maadhimisho ya siku za afya na lishe kila robo kulingana na mwongozo uliopo ili kufikisha elimu ya Lishe kwa jamii.
Kikao hicho kilicho fanyika leo Jumatano Agosti 9,2023
kililenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuona wapi wamefanya vizuri na wapi hawakufanya vizuri na kuweka mikakati ya kuboresha pale palipo na changamoto katika utekelezaji wa afua za Lishe kama ambavyo Wakuu wa Mikoa walisaini na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia Wakuu wa Wilaya walisaini na Wakuu wa Mikoa
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameagiza Halmashauri zote Shinyanga zitumie vikao vyote vya kikanuni kuweka ajenda ya lishe ili iweze kujadiliwa ambapo watafanya tathimini ya wapi wamefikia na wapi wamekwama waweze kuboresha huku akiwaagiza Maafisa Lishe wote waende kwa wananchi kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara wasikae ofisini.
"Katika hili, naelekeza afisa lishe wote kwenda kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao ambapo mtafanya mikutano na hapo ndiyo mtaweza kutoa elimu kwa wananchi wetu, msikae ofisini nendeni kwa wananchi mkaifanye kazi hii naagiza," amesisitiza Mhe. Mndeme.
Pia ameagiza fedha za lishe zitolewe kulingana na mpango kazi uliopo ili kutoathiri utekelezaji wa shughuli za lishe, Vijiji na Mitaa vyote Mkoa wa Shinyanga kufanya maadhimisho ya siku za Afya na lishe kila robo kulingana na mwongozo uliopo ili kufikisha elimu ya Lishe kwa jamii.
"Leo tupo hapa kwa ajili kufanya kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe mkoani kwetu ambapo kwa ujumla hali ipo vizuri sana, lakini jambo moja muhimu sana la kuzingatia ni kuwekea mkazo siku ya usafi wa mazingira ambapo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi wananchi washirikishwe kufanya usafi kwa dhati kabisa na wawe wanakumbushwa kwa matangazo," amesema Mhe. Mndeme.
Kando na hayo, Mhe. Mndeme amesisitiza juu ya kutengwa kwa Shilingi 1000/= kwa kila mtoto ambapo itatekelezwa kwenye afua za lishe jambo ambalo litaimarisha zaidi afya zao.
Katika hatua nyingine amesema Katika Mkoa wa Shinyknga Takwimu za lishe zilizotolewa na Wizara ya Afya kupitia Utafiti wa Taifa wa Masuala ya Afya na Lishe wa mwaka 2022, umeonyesha kuwa Udumavu kwa watoto chini ya miaka 5 umepungua kutoka asilimia 32.1 hadi Asilimia 27.5, ukondefu kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 1.3.
"Hii inaonyesha kuwa juhudi zetu za kupambana na utapiamlo zinazaa matunda. Hata hivyo kiwango hiki cha Udumavu bado ni kikubwa hivyo, tuendelee kusimamia utekelezaji wa mkataba wa lishe katika maeneo yetu",amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika hatua nyingine Mhe. Mndeme amewapongeza waandishi wa habari wote Mkoani Shinyanga kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhabarisha na kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na nje ya mkoa pia, jambo ambalo limepelekea jamii kuelimika sana na hivyo kusaidia kuimarisha afya zao, usafi wa mazingira na kupendezesha miji sambamba na kuelimisha umma juu ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa wananchi wake.
Katika kikao hicho wajumbe wa lishe mkoa wamewasilisha taarifa kutoka katika kila Wilaya ambapo kwa ujumla imeonesha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ni nzuri sana kwa kuwa zimekuwa na alama nzuri zote.
0 Comments