Ticker

6/recent/ticker-posts

RASILIMALI WATU NA FEDHA VYAPEWA KIPAUMBELE SADC

Na. Peter Haule, WF, Luanda-Angola

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imejipanga kuwekeza katika rasilimali watu na fedha ili kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Tamko la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu uwekezaji huo lililotolewa jijini Dar Es Salaam mwezi Julai 2023.

Hayo yamebainishwa jijini Luanda, Angola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioshirikisha nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Dkt. Tax alisema kuwa tamko la Dar Es Salaam limeainisha masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ambayo yameendelea kujadiliwa katika Mkutano wa 43 wa SADC ili kuhakikisha kuwa, katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahusu umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo endelevu ya viwanda, tamko la Dar Es Salaam linakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.

“Suala la uwekezaji katika rasilimali watu, suala la uendelezaji wa rasilimali watu katika kuendeleza uchumi, ni vitu ambavyo tunaendelea kuvisukuma kama ilivyokuwa kwenye mkutano jijini Dar es Salaam ambapo Rais wetu alikuwa Mwenyekiti wa mkutano ulioangazia masuala ya rasilimali watu uliofanyika Tanzania”, alieleza Dkt. Tax.

Awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Bw. Elias Magosi alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma kasi ya muingiliano, uendelezaji wa viwanda na upatikanaji wa masoko lakini pia nje ya nchi hizo.

Alisema kuwa uondoaji wa vikwazo hivyo, utaifanya kanda ya SADC kuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda wa 2020-2030 na dira ya kanda hiyo ya 2050.

Alisema kuwa, licha ya changamoto zinazoikabili dunia, kama mabadiliko ya tabianchi na mgogoro wa Urusi na Ukraine ambazo zimesababisha athari nyingi kwenye Kanda ya SADC, Jumuiya hiyo imefanikiwa kuziwezesha nchi wanachama kupata masoko ya kikanda na kimataifa ambapo nchi zilizonufaika na masoko hayo ni pamoja na Tanzania ambayo ilipata soko la parachichi katika nchi za China, India na Afrika Kusini.

Bw. Magosi aliendelea kueleza kuwa, kwa uratibu wa Sekretarieti ya SADC, nchi wanachama zimefanikiwa kupunguza msongamano wa magari, muda na gharama za usafirishaji katika baadhi ya mipaka, hususan yenye vituo vya pamoja vya mipakani (one stop border post-OSBP) kama Nakonde/Tunduma kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia.

Kwa upande mwingine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Angola.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya wataalam ambapo kwa Tanzania viliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban. Aidha mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) (kulia) akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Luanda, Angola, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa tatu kulia) akiwa na wajumbe wengine kutoka Tanzania kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika Luanda, Angola.
Afisa Dawati la SADC kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Charles Kato, wakipitia taarifa kabla ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika Luanda, Angola.
Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina (kulia) na Afisa Dawati la SADC kutoka Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Zainabu Turuka, wakipitia taarifa kabla ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika Luanda, Angola.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Luanda, Angola, akizungumza jambo wakati wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania kilichopitia taarifa mbalimbali kabla ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) (kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania kilichopitia taarifa mbalimbali kabla ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Luanda, Angola.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Antipas Nyamwisi (kulia) akikabidhi uenyekiti wa baraza hilo kwa Waziri wa Uhusiano wa Nje wa Angola, Mhe. Téte António, wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, Luanda Angola.
Wajumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza hilo, Luanda, Angola ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023.
Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakishiriki mkutano, Luanda Angola.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WF, Luanda, Angola)

Post a Comment

0 Comments