Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mabalozi kufuatilia utekelezaji wa Mikataba na Hati za Makubaliano zinazotokana na ziara za viongozi ndani na nje ya nchi.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo katika hafla ya kuwaapisha Mabalozi wateule iliyofanyika Ikulu, Chamwino.
Aidha, Rais Samia amesema ufuatiliaji huo uende sambamba na utekelezaji wa makubaliano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali yanayotokana na Tume za Pamoja za Ushirikiano na Mashauriano ya Kidiplomasia.
Vile vile, Rais Samia amewataka Mabalozi kuibua masuala ya ushirikiano katika vituo vyao vya kazi na kutafuta fursa mbalimbali ikiwemo katika sekta ya uwekezaji, utalii pamoja na mahitaji ya ‘diaspora’.
Rais Samia pia amewataka Mabalozi kufanya kazi kwa kuzingatia Dira ya Ajenda za Maendeleo za kimataifa na kitaifa ikiwemo falsafa ya 4Rs (Maridhiano, Ustahamilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya) kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaandaliwa mfumo utakaoingiza maelekezo ya ziara za viongozi wa ndani na nje ya nchi.
Rais Samia ameongeza kuwa mfumo huo utaonesha jukumu la kila wizara kwenye makubaliano yaliyofikiwa ili kuweza kupima utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi, Mabalozi Wateule pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya Uapisho iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 16 Agosti, 2023.
0 Comments