Serikali imesema Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) umeweka msingi wa mipango na bajeti shirikishi ya usimamizi wa mazingira katika ngazi zote na kuzingatia sekta mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati wa kikao cha kuwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mpango huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma tarehe 23 Agosti, 2023.
Amesema kwa kutambua na kuzingatia fursa na changamoto zilizopo, Ofisi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje kuhakikisha maeneo ya kipaumbele yaliyobainishwa kwenye Mpango yanatekelezwa na kujumuishwa kwenye mipango yao ya utekelezaji.
Dkt. Jafo amesema kuwa Mpango Kabambe unatekelezwa kwa kuzingatia sekta muhimu kama Kilimo ambayo uwekezaji mkubwa umefanyika ikiwemo uchimbaji wa malambo kwa ajili ya umwagiliaji katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa kupanda kwa Bajeti ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 261 hadi zaidi ya shilingi bilioni 900 kunaakisi kazi kubwa inayofanyika mathalan shughuli za umwagiliaji zinachangia katika upande wa mazingira.
“Leo hii tunaposema ujenzi wa malambo 114 ni almost shilingi bilioni 236, kwa kweli tumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani huo ni uwekezaji mkubwa sana na anachozungumza kule katika mikutano ya kimataifa ndio hiki ambacho kinaonekana sasa,“ alisema.
Tayari Wizara ya Kilimo imetoa mafunzo kuhusu kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima 1,500 katika Halmashauri za Hanang, Kongwa, Kilombero, Kahama, Babati, Makambako, Ludewa, Makete, Kyela, Mbinga na Nyasa na maafisa ngazi ya halmashauri 30 katika za Tarime Mji, Rorya na Serengeti.
Aidha, Dkt. Jafo alitaja sekta nyingine kama Nishati ambapo uwekezaji mkubwa wa nishati safi ya kupikia unaendelea kufanyika ikiwemo ni sehemu ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa yanayochangiwa na ukataji miti.
Hali kadhalika, alibainisha kuwa uchimbaji wa malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo ni hatua mojawapo inayosaidia kupunguza vitendo vya baadhi ya wafugaji kunyweshea mifugo yao kwenye vyanzo vya maji.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo kwa wafugaji 184 kuhusu ufugaji endelevu unaozingatia hifadhi ya mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, elimu imetolewa kwa wavuvi 204 Bwawa la Nyumba ya Mungu (87) na Bwawa la Mtera (117) kuhusu kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na uvuvi usiokuwa endelevu.
Alisema Uchukuzi umechangia katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mazingira kwani mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayotumia umeme badala ya mafuta mazito utasaidia katika kupunguza hewa ya ukaa hivyo kulinda mazingira.
“Jamii inaendelea kuhamasishwa kuthamini mazingira na kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi, ustawi ya jamii na Tanzania ya kijani,“ alisisitiza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma tarehe 23 Agosti, 2023.
0 Comments