Ticker

6/recent/ticker-posts

MENEJIMENTI YA HIFADHI YA TAIFA KATAVI YATAKIWA KUTANGAZA UTALII NA MAENEO YA UWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameitaka Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Katavi kuainisha maeneo ya uwekezaji huku akisisitiza utangazaji wa kimkakati katika maeneo hayo ufanyike ili kuwavutia Wawekezaji wa ndani na nje nchi kuwekeza katika Hifadhi hiyo

Ametoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya Hifadhi hiyo, ambapo amesema utangazaji wa maeneo hayo utawavutia Wawekezaji kuwekeza katika ujenzi wa huduma za malazi ya watalii.

"Ainisheni maeneo hayo kwani Wawekezaji wengi wanataka kuwekeza katika Hifadhi hii " Mhe. Masanja amesisitiza.

Akizungumzia faida ya kutangaza maeneo watakayoainisha, Mhe.Masanja amesema miundombinu itaboreka pamoja na mazingira yatawavutia watalii wengi kuja kutembelea na kulala hifadhini humo

Katika hatua nyingine, Mhe.Masanja ameendelea kuwasisitiza Wananchi kuacha kuvamia maeneo ya Hifadhi huku akiwataka wahifadhi kuendelea kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa maeneo hayo kitaifa na kimataifa.

"Ili kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na Wananchi wetu, Nawaomba nendeni mkatoe elimu kwa wananchi wasisogelee maeneo ya hifadhi na hapo walipo wasiendelee kuongeza maeneo" Mhe. Masanja amesema

Hifadhi ya Taifa Katavi ni hifadhi ya tano kwa ukubwa kati ya hifadhi 21 nchini ikiwa na kilomita za mraba 4,471.

Post a Comment

0 Comments