Ticker

6/recent/ticker-posts

MASANJA AZINDUA HOTELI YA HOME GROUND KUKUZA HUDUMA ZA MALAZI KWA WATALII MKOANI KATAVI

*Asisitiza ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi katika utoaji huduma za kitalii**_

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amezindua hoteli ya Home Ground katika Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi itakayosaidia kukuza Mtandao wa Utalii katika eneo la huduma na malazi kwa watalii wanaokuja nchini.

Akizungumza jana Agosti 6,2023 katika uzinduzi huo, Mhe. Masanja amesema kuwa uwekezaji wa hoteli hiyo unaenda kusaidia Hifadhi ya Taifa Katavi ambayo ni moja kati ya hifadhi ya tano kwa ukubwa nchini ikiwa yenye kilomita za mraba 4,471.

Ameongeza kuwa uzinduzi wa hoteli hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za malazi nchini.

“Tukio hili linaonesha dhahiri umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutoa huduma za kitalii na pia linaunga mkono juhudi thabiti za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kama alivyoeleza katika uzinduzi wa filamu ya "The Royal Tour " *“tunapenda kuwakaribisha wawekezaji wengine kwani Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutangaza utalii duniani na kufungua milango kwa nchi nyingi kutembelea Tanzania* ” Mhe. Masanja amesema.

Aidha, ametumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uwekezaji huo mkubwa uliofanyika, huku akisema idadi na viwango vya huduma za malazi imeongezeka.

"Sisi kama Serikali tutazidi kuweka mazingira wezeshi ili kudumisha ushirikiano mkubwa katika kukuza na kuongeza idadi wa watalii wanaofika katika hifadhi hii ya Katavi, wekezeni kwenye huduma za malazi " amesisitiza Mhe.Masanja.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Hoteli ya Home Ground, Mhe. William Mbogo amesema ujenzi wa Hoteli hiyo uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5 ulianza mwaka 2019 na unatarajiwa kutumia takribani bilioni 4 mpaka kukamilika kwake.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kuchangia katika mapato ya Serikali kwa kodi mbalimbali inayolipa lakini pia umetoa ajira kwa vijana takribani 40 wa Kitanzania.

Mbogo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuboresha miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza ndani ya hifadhi hiyo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), akizindua Hoteli ya Home Ground, Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi Mhe. Willian Mbogo pamoja na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wakishuhudia uzinduzi huo uliofanyika katika Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Home Ground, Bw. Kevin Mbogo(wa pili kushoto)pamoja na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wakikagua mojawapo ya chumba cha hoteli ya Home Ground kabla ya uzinduzi wa hoteli hiyo uliofanyika katika Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(wa tatu kushoto) akizungumza na wahudumu wa hoteli ya Home Ground ambapo amewataka kuwa wakarimu wanapohudumia wageni ili kuwavutia waweze kurudi kwa mara nyingine. Kulia kwake ni Mkurugenzi  Mtendaji wa Hoteli ya Home Ground, Bw. Kevin Mbogo na kushoto kwake ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, Mhe. Taska Mbogo.Wengine ni baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wakishuhudia.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(katikati) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi wa Hoteli ya Home Ground, Mhe. William Mbogo (wa tatu kutoka kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Home Ground, Bw. Kevin Mbogo(wa pili kutoka kulia)pamoja na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali.

Post a Comment

0 Comments