Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUWASAIDIA WAUMINI KUMALIZA MIGOGORO YA NDOA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuwasaidia waamini kumaliza migogoro ya ndoa na mirathi kwa amani pasipo kuathiri watoto.

Makamu wa Rais amesema hayo aliposhiriki Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana Askofu Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Amesema migogoro ya ndoa na mirathi imeziathiri familia nyingi na kuwaacha akina mama na watoto katika madhira makubwa ikiwemo ongezeko la watoto wa mitaani, ongezeko la familia za mzazi mmoja pamoja na wajane kunyang’anywa mali walizoachiwa na wenza wao kinyume na mafundisho ya dini.

Makamu wa Rais amesema sehemu kubwaa ya mmomonyoko wa maadili unaoshuhudiwa kwa sasa umechangiwa na malezi mabaya na kuvunjika kwa taasisi ya ndoa hivyo amewahimiza wazazi na walezi kutekeleza wajibu wa kuwalea Watoto na vijana katika maadili ili kuepuka athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika familia.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Takwimu kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonesha jumla ya talaka 442 zilisajiliwa mwaka 2019, talaka 511 zilisajiliwa mwaka 2020 na talaka 550 zilisajiliwa mwaka 2021.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kutambua umuhimu wa kulinda na kudumisha amani, umoja na uhuru wa Taifa.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani amechukua hatua za makusudi za kuimarisha amani, demokrasia, umoja, uhuru na mshikamano wa Taifa.

Ameongeza kwamba Rais ameonesha kwa vitendo dhamira yake ya kujenga umoja wa kitaifa ikiwemo kushiriki shughuli za vyama vingine vya siasa na madhehebu mbalimbali ya kidini.

Halikadhalika amewahimiza waamini wote kutambua umuhimu kutunza mazingira na kujiepusha na tabiawatu zinazopelekea uharibifu wa mazingira.

Amesema licha ya jitihada kubwa za nchi na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, bado tatizo ni kubwa na athari zake zinasababisha maafa makubwa kwa uhai wa mwanadamu na viumbe wengine.

Makamu wa Rais amesema Serikali inathamini kazi nzuri inayofanywa na Taasisi za kidini katika kutunza, kulea na kusomesha Watoto yatima, watu wenye mahitaji maalum pamoja na wazee.

Pia amesema serikali inapongeza mchango maridhawa wa dini katika kuhimiza maadili mema na kudumisha amani, upendo na mshikamano katika Taifa.

Aidha amewasihi kuendelea kuliombea taifa na viongozi wa Serikali ili waweze kuwa na busara na unyenyekevu katika kuwatumikia Watanzania.

Makamu wa Rais amemsihi Askofu Luzineth Kingamkono wa Dayosisi hiyo ya Mpwapwa kufanya kazi kwa bidii, unyenyekevu na uaminifu na kujiepusha na tamaa ya mali na madaraka.

Aidha amemuasa kutokatishwa tamaa na makwazo mbalimbali atakayopambana nayo katika utumishi na wito wake.

Mara baada Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana, Askofu Luzineth Kingamkono amesema Dayosisi hiyo itaendelea kuunga mkono adhma ya serikali ya kupiga vita umasikini, maradhi na ujinga kwa kutoa huduma za kijamii kama vile uwepo wa shule na zahanati zinazomilikiwa na Dayosisi hiyo Wilayani Mpwapwa.

Amesema Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa wana imani kubwa na serikali kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaongoza taifa kwa amani, upendo na utulivu hivyo wataendelea kuwaombea viongozi wa serikali na kuliweka taifa mikononi mwa Mungu wakati wote.

Aidha Askofu Kingamkono amesema uwepo wa umoja wa kitaifa ndio chachu ya Tanzania kupiga hatua za maendeleo hivyo amewasihi viongozi wa dini kuwapongeza na kuwaombea viongozi wa serikali ili waweze kutimiza majukumu yao kiufanisi.

Ameongeza kwamba Dayosisi hiyo inashirikiana na mashirika yasio ya kiserikali katika kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti na usafi wa mazingira.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa ameipongeza serikali kwa jitihada mbalimbali inazofanya katika kuwaleta wananchi maendeleo ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa.

Askofu Mndolwa ametoa wito kwa serikali kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara kiwango cha lami kuingia katika Wilaya ya Mpwapwa ili kurahisisaha huduma kwa wananchi na viongozi viongozi wa dini wanapotoa huduma za kiroho.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dkt. Maimbo Mndolwa mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Tarehe 27 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi na Waumini wa Kanisa la Anglikana mara baada ya Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Tarehe 27 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Askofu Luzineth Kingamkono mara baada ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kuwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa wa Kanisa la Anglikana katika Ibada iliofanyika katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma leo tarehe 27 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakishiriki katika Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Tarehe 27 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na aliyekuwa Mlezi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa Askofu Dickson Chilongani wakati alipowasili katika Dayosisi hiyo kushiriki Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Tarehe 27 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dkt. Maimbo Mndolwa (watatu kutoka kushoto) Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa Luzineth Kingamkono (Wapili kutoka kulia), Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango (watatu kutoka kulia) pamoja na Maaskofu mbalimbali wa Kanisa la Anglikana mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Kuwekwa Wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana, Ibada iliofanyika Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Tarehe 27 Agosti 2023.

Post a Comment

0 Comments