******************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema kuwa moja ya malengo ya bodi hiyo kwa mwaka huu 2023 ni kuzalisha tani 60,000 kutoka tani 48,000 mwaka 2022.
Kambona amesema mwaka 2020 wakati TSB inapewa jukumu na serikali la kuhakikisha uzalishaji unapanda hadi kufikia tani 120,000 mwaka 2025, ilikuwa inazalisha tani 36,000 kwa mwaka na sasa hivi wamefunga mwaka 2022 kwa kuzalisha tani 48,000.
"Lengo letu ni kufikisha tani 60,000 na tayari hadi kufikia Juni mwaka huu tulikuwa tumeshazalisha tani 34,000. Kwa hiyo tunajiona kabisa tutamaliza mwaka 2023 kwa kuzalisha tani 60,000 bila wasiwasi,
"Jitihada zimeshafanyika ambapo serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya Bodi ya Mkonge kwa kuiwezesha kupata vyombo vya usafiri kwa ajili ya kushughulikia upatikanaji wa takwimu ambao ulikuwa kikwazo,
"Na ndiyo maana utaona sasa hivi takwimu zimepanda siyo kwamba Mkonge haukuwepo lakini takwimu zilikuwa hazikusanywi ipasavyo, kimsingi mabadiliko ni makubwa sana." amesema.
Akizungumzia takwimu za mapato Kambona amefafanua kwamba tangu serikali imechukua juhudi za kufufua zao la Mkonge mwaka 2019 na kutambulishwa kuwa zao la kimkakati, mauzo ya nje yameongezeka ambapo pekee yamefikia Dola za Marekani milioni 56 kutoka Dola milioni 42 kwa kipindi cha miaka miwili.
"Lakini mauzo ya ndani pia yaliongezeka kutoka sh bilioni 41 hadi sasa sh bilioni 43 kwa soko la ndani, kwa hiyo soko la nje limefanya vizuri zaidi yaani Mkonge mwingi umeuzwa zaidi nje kuliko ndani lakini mwisho wa siku takwimu zimepanda," amefafanua.
Pia amebainisha kwamba pamoja na hayo, wastani wa mauzo ya singa za Mkonge (fiber) tani moja ni takribani Sh 3,500,000 kwa madaraja ya juu.
0 Comments