Ticker

6/recent/ticker-posts

Jamii ya Wafugaji wapewa elimu kuepuka migogoro ya Malisho.

Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.

Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini limetoa elimu kwa viongozi wa Wafugaji toka Mikoa ya Arusha na Manyara wanaozunguka hifadhi za taifa za Wanyama kuhusiana na namna bora ya kuepuka migogoro ya malisho wakati wa kiangazi.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU) Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua ametoa elimu hiyo mapema leo huko katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire Mkoani Manyara na kuwataka wafugaji kutumia kipindi hiki ambacho hakina ukame kujiandaa vyema na kutenga maeneo ya malisho ambayo watayatumia kipindi cha kiangazi.

Kamanda Pasua amebainisha kuwa Jeshi hilo limeamua kuwatumia Viongozi hao wa Mila maarufu ‘’Legwanani’’ ili wafikishe ujumbe huo kwa jamii nzima ya wafugaji ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ya kugombania maeneo ya malisho.

ACP Pasua amefafanua kuwa kupitia elimu ambayo imetolewa ni imani yake kuwa hakutakua na migogoro baina ya wafugaji, wakulima lakini pia maeneo ya hifadhi za Taifa.

Kwa upande wake Bwana Julius Mariki toka wilayani Monduli amesema changamoto kubwa waliyonayo wafugaji ni mabadiliko ya hali hewa na tabia nchi ambapo amekiri kuwa hakuna mbadala uliopo zaidi ya elimu kuendelea kutolewa kwa jamii hizo za kifugaji ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya mara kwa mara.

Ameongeza kuwa kazi ya Viongozi wa mila pamoja na mambo mengine ni kusimamia amani, haki pamoja na maeneo ya malisho ambapo kwa ushirikiano mzuri walionao na Jeshi la Polisi migogoro itakwenda kumalizwa kabisa.

Kiongozi mwingine toka jamii ya wafugaji amesema wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanalinda hifadhi hizo za Taifa kwa kutoa taarifa kwa wahalifu wote watakaobanika kuingia katika hifadhi hizo kufanya ujangangili.

Post a Comment

0 Comments