Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameupongeza uongozi wa Wakala ya Barabara nchini (TANROAD) pamoja na Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi mzuri na kukamilisha ujenzi wa barabara ya mchepuko katika eneo la mlima wa Inyala mkoani Mbeya.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikagua barabara ya mchepuko katika Mlima Inyala iliogharimu shilingi bilioni 6.9 leo tarehe 01 Agosti 2023.
Amesema eneo hilo lilikuwa likikabiliwa na ajali nyingi zilizogharimu Maisha ya watu hivyo kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia katika kukabiliana na adha hiyo.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuwa waangalifu na kufuata sheria za usalama barabarani ili kunusuru Maisha ya watumiaji wa barabara.
Ametoa wito kwa madereva kujenga utaratibu wa kukagua magari mara kwa mara ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza kutokana na ubovu wa vyombo vya moto.
Aidha Makamu wa Rais amewataka askari wa usalama barabarani kufanya kazi kwa uadilifu kwa kusimamia sheria za usalama barabarani ili kulinda Maisha ya wananchi wanaotumia barabara hizo.
Septemba 11 mwaka 2022 Makamu wa Rais alitembelea eneo la Inyala na kuagiza mambo mbalimbali ili kukabiliana na ajali zilizokuwa zinajitokeza katika eneo hilo ikiwemo kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya mchepuko katika mlima Inyala, kupanua ukubwa wa barabara kutoka mita 6.7 hadi mita 10.5 pamoja na kuweka taa za barabarani katika eneo la kukagulia magari.
Halikadhalika Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa Zahanati ya Shamwengo iliopo eneo la Inyala ambayo mwaka 2022 aliagiza ikamilishwe ili kusaidia majeruhi waliokuwa wanapata ajali katika mlima Inyala.
Amesema ameridhishwa kwa kukamilika kwa zahanati hiyo na kuwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujitoa kusaidia watu waliokuwa wakipata ajali katika eneo la mlima Inyala.
Ameongeza kwamba serikali itapeleka shilingi milioni 110 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa katika zahanati hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Barabara ya mchepuko katika mlima Inyala mkoani Mbeya leo tarehe 01 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Zahanati ya Shamwengo iliopo eneo la Inyala mkoani Mbeya leo tarehe 01 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha shamwengo mara baada ya kutembelea zahanati ya Kijiji hicho leo tarehe 01 Agosti 2023.
0 Comments