Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio (katikati) akimkabidhi kitanda na godoro, Katibu Tawala wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Saidi Kitinga (kushoto) kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio (wa pili kushoto) akimkabidhi kitanda na godoro, Katibu Tawala wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Saidi Kitinga (kushoto) kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Na MWANDISHI WETU - MALUNDE 1 BLOG
Benki ya NMB Kanda ya Magharibi imetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 25.8 (Tshs 25,844, 075/=) katika zahanati ya Lyabukande na Mwabenda pamoja na Hospitali ya wilaya ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Benki hiyo katika maendeleo ya jamii kwani ina wajibu wa kuhakikisha jamii inayowazunguka inafaidika kutokana na faida wanayoipata.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 7,2023 wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio amesema Benki ya NMB ni kinara katika kujali na kujihusisha na masuala mbalimbali ya jamii hapa nchini na kwamba changamoto za sekta ya afya Tanzania kwa benki ya NMB ni jambo la kipaumbele, na hii ni kutokana na ukweli kwamba afya ni mtaji wa maendeleo kwa taifa lolote hapa duniani.
Amesema katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga wamekabidhi Wheel chairs 4, Stretchers 4,Vitanda vya hospitali 10,Godoro za Hospitali 10, Mashuka 50, vyenye thamani ya Tshs 12,347,350/=, kwa Zahanati ya Lyabukande ni Wheel chairs 2, Vitanda vya kujifungulia 2 Vitanda vya Hospitali 5, Magodoro ya hospitali 5, mashuka 50,vyenye thamani ya Tshs 6,852,425/= na kwa zahanati ya Mwabenda wheel chair 2, vitanda vya kujifungulia 2, Vitanda vya Hospitali 5, magodoro ya hospitali 5, mashuka 50,vyenye thamani ya Tshs 6,852,425/= .
"Tulipopata maombi haya ya kuchangia maendeleo ya afya katika Wilaya ya Shinyanga, tulifarijika na kuamua mara moja kuja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hii muhimu kwa jamii yetu. Na hasa katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na hususani katika hospitali ya Wilaya ya Shinyanga, Zahanati ya Lyabukande na Zahanati ya Mwabenda. Jumla ya msaada huu tuliotoa una thamani ya Tshs 25,844,075",ameeleza Urio.
"Benki ya NMB imekuwa ikipokea maombi mengi sana ya kuchangia katika miradi ya jamu, lakini benki imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya, na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga. Benki NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii. Ni kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotunzunguka",ameeleza Urio.
"Tunatambua juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kusimamia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa nguvu zote kwa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hizi mjini na vijijini; hatuna budi kuipongeza Serikali kwa hilo. Pamoja na makubwa mengi yanayofanywa na Serikali, sisi kama wadau tunao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii zetu kwani jamii hizi ndio zimeifanya benki ya NMB kuwa hapa ilipo na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini. Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka, kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu",ameongeza Urio.
Aidha amebainisha kuwa, kwa miaka kadhaa sasa, NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu (madawati na vifaa vya kuezeka), afya (vitanda, magodoro yake na vifaa vingine vya kusaidia matibabu) na kusaidia majanga yanayoipata nchi ya Tanzania.
Urio amefafanua kuwa Benki NMB ndiyo benki inayoongoza nchini huku tukiwa na matawi 229 , mashine za ATM zaidi ya 780 nchi nzima, NMB Wakala zaidi ya 20,000 pamoja na idadi ya wateja zaidi ya milioni 6 idadi ambayo ni hazina kubwa ukilinganisha na benki nyingine hapa nchini lakini pia NMB imezifikia Wilaya zote nchini kwa asilimia 100% na tunaendelea kuboresha huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ili kuwafikia wateja wengi zaidi kwa njia rahisi na salama.
Akipokea vifaa tiba hivyo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Katibu Tawala wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Saidi Kitinga ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo katika sekta ya afya huku akiwataka wahudumu wa afya kuvitunza vifaa hivyo ili viwe na manufaa na kuleta tija iliyokusudiwa.
Nao Diwani wa kata ya Iselamagazi Isack Sengerema na diwani wa Kata ya Lyabukande Luhende William Kawiza wameishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuikumbuka sekta ya afya katika wilaya ya Shinyanga.
0 Comments