Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA MJI WA SERIKALI

*Aagiza ifikapo Oktoba mwaka huu uwe umekamilika

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kuwa ifikapo Oktoba mwaka huu, mradi wa majengo ya wizara mbalimbali unaoendelea katika mji wa Serikali uwe umekamilika na kuwekwa samani, ili azma ya Serikali ya watumishi kuhamia kwenye majengo hayo ifikapo Januari Mosi, 2024 itimie

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi huo wahakikishe wananunua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini lengo likiwa ni kuokoa fedha za kigeni pamoja na kuongeza tija katika uwekezaji.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 03, 2023) baada ya kukagua ujenzi wa Mji wa Serikali na uwanja wa Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma. “Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutaka kuona watumishi wote waliohamia Dodoma wanafanya kazi kwenye majengo rasmi.”

“Tafuteni mbinu za kiufundi za kukamilisha majengo haya kwa wakati bila kuathiri viwango ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi huu usiku na mchana, tunataka tumalize majengo haya, Watanzania wanataka kuona majengo yanakamilika na kutumika.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo watumie bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini. “Rais Dkt. Samia amesisitiza kuhusu uwekezaji na amekuwa akialika wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya bidhaa mbalimbali hapa nchini ikiwemo marumaru (tiles). Tutumie bidhaa zao badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.”



Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema mbali na mradi wa ujenzi wa majengo ya wizara pia mradi mwingine unaotekelezwa katika eneo hilo ni ujenzi wa uwanja wa Mashujaa ambao utakuwa na mnara utakaoongoza kwa urefu barani Afrika. Mnara huo utakuwa na urefu wa mita 110.



Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi alisema watahakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. “Ifikapo Septemba 30, 2023 mradi huo utakuwa umekamilika.”




Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (kulia kwake ) wakati alipokagua ujenzi wa jengo la Wizara hiyo akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, eneo la Mtumba jijini Dodoma, Julai 3, 2023. (Picha na Ofisi ya Wairi Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha majumuisho baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma, Julai 3, 2023. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua na kupewa maelezo kuhusu ujenzi wa jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma, Julai 3, 2023. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda, wa tatu kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama na wa nne kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments