Ticker

6/recent/ticker-posts

WAAJIRIWA SEKTA BINAFSI WATAKIWA KUZINGATIA KIMA KIPYA CHA MSHAHARA

Na: Mwandishi Wetu - Dodoma

OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Kazi imewataka waajiri wa sekta binafsi nchini kuzingatia kima kipya cha chini cha mshahara kilichotangazwa na serikali mwaka huu kwa kuwa ni takwa la kisheria.
Kima hicho kilitangazwa katika kupitia tangazo la serikali namba 687 na kilianza kutumia Januari mosi, 2023 na kimewekwa kwenye sekta kuu 13.

Kamishna wa Kazi Msaidizi, Mahusiano kazini wa Ofisi hiyo, Andrew Mwalwisi ameyasema hayo Julai 19, 2023 alipokuwa akitoa elimu kwa umma jijini Dodoma kuhusu sheria na miongozo ya kazi.

Amesema kwa sekta ya kilimo ni Sh.140,000, afya (Sh.195,000), mawasiliano imegawanyika kuna sekta ya huduma za mawasiliano (Sh.500,000), huduma za utangazaji na vyombo vya habari, posta usafirishaji vifurushi ni (Sh.225,000) kwa anayeanzia chini kabisa.

“Kazi za majumbani imekuwa changamoto kidogo ya kutoelewa kwa majumbani hii sekta imegawanyika kwenye makundi manne kuna wafanyakazi wa kazi za ndani walioajiriwa na wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wanapaswa kulipwa Sh. 250,000, kuna walioajiriwa na Maafisa wenye stahiki Sh. 200,000, kuna wanaoishi katika kaya ya mwajiri hawa ndo wengi ndo wengi wanapaswa kulipwa Sh. 120,000 na wanaokwenda na kurudi Sh.60,000,” amesema.

Alibainisha hoteli kubwa za kitalii kima cha chini ni Sh.300,000, za kati Sh. 180,000 ,migahawa, nyumba za kulala wageni na baa Sh. 150,000, ulinzi binafsi (kwa kampuni kubwa Sh.220,000 na madogo ni Sh. 148,000), sekta ya nishati (kampuni za kimataifa 592,000 na madogo ni Sh. 225,000), Usafirishaji (wa anga Sh. 390,000, utoaji mizigo na usambazaji Sh.360,000, nchi kavu kwa madereva wao wanapaswa kima cha chini kiwe Sh. 300,000 kwa mwezi.

“Kuna sekta ya ujenzi (daraja la kwanza Sh. 400,000, la pili hadi la nne sh.360,000, la tano hadi la saba Sh. 320,000), sekta ya madini (uchimbaji na utafutaji madini Sh. 500,000, wenye leseni za wachimbaji wadogo sh. 300,000, biashara sh.450,000, madalali sh. 250,000), huduma za shule binafsi ni Sh. 207,000, sekta ya biashara na viwanda Sh.150,000, taasisi za fedha Sh. 592,000, uvuvi na huduma ya baharini sh.238,000 na sekta nyinginezo ambazo hazijatajwa kwenye makundi hayo ni Sh. 150,000 kwa mwezi,” amesema.
Kamishna wa Kazi Msaidizi anayeshughulikia Mahusiano kazini Bw. Andrew Mwalwisi akitoa elimu kwa umma jijini Dodoma kuhusu sheria na miongozo ya kazi leo Julai 19, 2023.

Post a Comment

0 Comments