Na Ezekiel Kamwaga
BAADA ya Serikali kutangaza gharama za ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa zilizokadiriwa kufikia shilingi bilioni 31, baadhi ya wadau wa michezo wamehoji kuhusu gharama hizo kubwa za ukarabati. Haya ni maelezo mafupi yanayojibu maswali yaliyoibuliwa na wadau kuhusu kiwango hicho.
Kwa nini uwanja unakarabatiwa?
Tangu Uwanja wa Benjamin Mkapa ukamilike mwaka 2007, haujawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa kama ambavyo inatakiwa. Kwa mfano, viti vilitakiwa kubadilishwa baada ya miaka 10 lakini jambo hilo halikufanyika. Eneo la kukimbilia riadha lilitakiwa kufanyiwa ukarabati tangu mwaka 2012, lakini hilo halijafanyika hadi sasa.
Vitu kama mfumo wa vyoo vinavyotumika uwanjani, taa zinazotumika ambazo zimepitwa na wakati kulingana na mahitaji ya sasa, vifaa vya zimamoto na uokoaji na miundo ya tehama vinahitaji vyote kufanyiwa ukarabati ili uwanja huo ubaki na heshima yake kama uwanja bora katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Uwanja wa Mkapa kwa sasa ndiyo unatambulika kama uwanja bora katika ukanda huu wa Afrika na ndiyo sababu sasa ni wa uwanja wa nyumbani wa mataifa kama Burundi, Somalia, Sudan Kusini na Kenya. Ili kubaki katika sifa yake hiyo, ukarabati mkubwa ulitakiwa kufanyika.
Matengenezo ni jambo la lazima
Lakini ukarabati huu unafanyika pia kukidhi masharti yaliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili timu za Tanzania ziweze kushiriki katika mashindano mapya ya Super League. Timu ya Tanzania, Simba SC ndiyo timu pekee kutoka Afrika Mashariki iliyopata nafasi ya kushiriki mashindano hayo. Marekebisho karibu yote yanayotakiwa kufanywa yanakidhi masharti. Bila kukidhi masharti hayo, Simba au timu yoyote ya Tanzania -kwa vigezo hivyo, isingeruhusiwa kushiriki mashindano hayo.
Ni jambo zuri pia kwamba ukarabati huu umetangazwa kufanyika katika wakati ambao nimeelezwa timu ya wakaguzi kutoka CAF inakuja nchini kuangalia maendeleo ya mapendekezo yao kuhusu maboresho ya uwanja huo. CAF, kwa sasa, inautazama uwanja huo kama mboni kwa sababu ndipo uzinduzi wa Super League na takribani viongozi wote wa juu wa mpira barani Afrika na duniani kwa ujumla watafika uwanjani kushuhudia tukio hilo.
Kuhusu gharama za Uwanja
Wapo wadau waliohoji iweje uwanja uliogharimu shilingi bilioni 50, ukarabati wake uwe shilingi bilioni 31? Kwanza, wakati uwanja unakamilika mwaka 2007, gharama ilikuwa dola milioni 56 za Marekani (sio bilioni 50 zinazosemwa). Hii maana yake ni kwamba, kama uwanja huu ungekuwa umejengwa mwaka huu, gharama yake ingekuwa takribani shilingi bilioni 137 za Tanzania. Kwa viwango hivyo vya mwaka 2007, marekebisho haya ya sasa ni sawa na shilingi bilioni 20.4. Hivyo, gharama ya uwanja huu kwa sasa inatakiwa iwe shilingi bilioni 137 kwa thamani ya dola ya wakati huu.
Kimsingi, kwa sasa gharama zilizo kwenye mitandao kwa nchi zinazotaka kujenga uwanja wa aina ya Benjamin Mkapa zinakadiriwa kuwa kati ya dola milioni 100 hadi milioni 160 (kati ya shilingi bilioni 240 hadi bilioni 350).
Mfano wa ukarabati wa viwanja ni Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Uwanja huo sasa unafanyiwa marekebisho makubwa utakaowezesha kuwa na uwezo wa kuingiza washabiki takribani 15,000. Kwa mujibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kiasi cha shilingi bilioni 15 zitatumika kwa ukarabati huo. Uwanja wa Mkapa unaingiza watazamani mara nne ya uwanja huo wa Amaan lakini gharama za marekebisho ni takribani mara mbili tu ya uwanja huo wa Zanzibar.
Mimi ni shabiki wa Liverpool ya Uingereza. Mwaka 2021, klabu iliamua kuongeza uwezo wa uwanja wa Anfield kuingiza washabiki kutoka 53,000 hadi 61,000 (sawa na kwa Mkapa). Gharama za marekebisho ya jukwaa litakalohusika, lile la Anfield Road Stand, imekadiriwa kufikia dola milioni 97 (sawa na takribani shilingi bilioni 237 za Tanzania). Haya ni marekebisho yanayohusu upande mmoja tu wa jukwaa kwa kuongeza viti 8,000. Kwa hiyo gharama hizi za ukarabati wa uwanja zinaendana na gharama za marekebisho makubwa yanayofanyika katika viwanja vingine duniani.
Nini hasa vinarekebishwa?
Takribani vitu 30 vitafanyiwa marekebisho kwa wakati mmoja. Vitu hivyo ni kama vile, vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji, chumba na maeneo ya waandishi wa habari, viti vyote vilivyo uwanjani, mfumo wa matangazo, luninga ya kisasa uwanjani, eneo la matajiri, lifti mbili mpya, mifumo ya tehama, mifumo ya vyoo, eneo la kuchezea mpira, magoli na nyavu, eneo la kupigia kona, eneo la kukimbia riadha, mfumo wa maji eneo la kuchezea, mgahawa, mfumo wa AC, mfumo wa umeme mfumo wa kisasa wa VAR.
Maeneo mengine ambayo ukarabati huu utayagusa moja kwa moja ni eneo la kukaa wachezaji wa akiba na benchi la ufundi, eneo la wageni mashuhuri, vyumba vya kupumzika vya watu mashuhuri, ofisi za ndani ya uwanja, chumba cha waamuzi, eneo la Gym, maboresho ya taa zote za uwanjani na eneo la kuingilia uwanjani.
Serikali italipia gharama zote?
Pamoja na umuhimu wa ukarabati huu, CAF inafahamu kwamba serikali nyingi za Afrika – ikiwemo Tanzania, zinakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi zinazohitaji rasilimali hii kidogo iliyopo. Hivyo, katika suala hili, serikali, CAF na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF) kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo watachangia gharama za ukarabati. Serikali haitatoa fedha zote.
Gharama za ukarabati ni kubwa?
Kwa vigezo vyovyote vile, shilingi bilioni 31 ni kiasi kikubwa. Lakini, ukilinganisha faida ya kufanya ukarabati huu na hasara ya kutofanya, ukarabati unaonekana ni wa muhimu zaidi. Kwa mfano, mshindi wa mashindano haya anatarajiwa kupata zawadi ya dola milioni 11.5 ( sawa na shilingi bilioni 28). Kama Simba au timu yoyote kutoka Tanzania itafanikiwa kutwaa Kombe hili – na hii si ndoto ya alinacha kwa sababu Yanga ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka huu, zawadi itakuwa sawa na ukarabati wote uliofanyika.
Hata kama timu ya Tanzania haitachukua kombe, Simba – na timu zingine za Tanzania zitakazokuja kupata nafasi ya kushiriki mashindano haya, kushiriki pekee kunaipa uhakika wa kupata shilingi bilioni nane kutoka CAF kila mwaka wa mashindano. Hii maana yake ni fedha za ukarabati huu zitajilipa kwa vilabu vyetu katika kipindi cha miaka minne tu ijayo.
Lakini tuangalie ukarabati wenyewe unahusu nini hasa. Chukulia mfano wa taa za uwanjani. CAF inataka kutumika kwa taa za mfumo wa kisasa wa LED ambazo zinawashwa na kuzimwa kidijitali. Taa hizo zinachukua sekunde chache tu kuwaka kulinganisha na taa zilizopo sasa ambazo zikizimika, hutumia kati ya dakika 15 hadi 20 kuwaka upya.
Uwanja wa Mkapa unahitaji wastani wa taa za LED 300 kufanya kazi zake ipasavyo. Gharama ya taa moja ya LED inakadiriwa kufikia kiasi cha shilingi za Tanzania milioni 12. Kwa sababu hiyo, gharama ya taa peke yake inaweza kufika takribani shilingi milioni 360.
Ukarabati huu unazungumzia takribani viti 45,000. Hapa unazungumzia gharama za kuanzia utengenezwaji na usafirishwaji wa mzigo wa makontena zaidi ya tisa yenye urefu wa takribani futi 40 kila moja. Gharama za ukarabati mkubwa wa kiasi hiki huwa ni kubwa na ndiyo sababu ni rahisi kusema kiasi hiki ni kikubwa lakini hakuna anayeweza kusema kwa yakini kidogo na kiasi gani na kingefanya nini.
Viwanja kama vyanzo vya mapato
Ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ni ukarabati unaolipa kiuchumi. Wakati Liverpool ilipoamua kukarabati uwanja wake wa Anfield, iliamua kuongeza viti takribani 8,500, huku zaidi ya nusu vikiwa ni eneo la matajiri. Kuongeza viti vya matajiri uwanjani kunaongeza mapato kwa uwanja kutokana na wanaoingia na mapato kwa wajasiriamali ambao huduma zao zitatumiwa na watu wenye ukwasi.
Kwa sasa, Uwanja wa Benjamin Mkapa unaingiza takribani shilingi bilioni tano kwa mwaka kupitia mechi za mashindano mbalimbali yanayofanyika uwanjani hapo. Sehemu kubwa ya mapato huenda kwa vilabu kama Simba na Yanga lakini kiasi cha walau kati ya shilingi bilioni 1.8 hadi bilioni mbili hubaki kwenye uwanja. Ukarabati huu utakapokamilika, uwanja utaweza kuingiza mapato kwa uwanja yanaweza kuzidi shilingi bilioni mbili kwa mwaka – kwa sababu ya faida ya kuwa na mashindano ya Super League ambayo hayakuwepo.
Uwanja wa Mkapa ni “sebuleni” kwetu
Uwanja wa Benjamin Mkapa umetangazwa na CAF kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Super League. Mechi hiyo itashuhudiwa na wapenzi wa soka barani Afrika na duniani kwa ujumla. Wageni hao watapata taswira halisi ya Tanzania kupitia kile watakachokiona uwanjani siku hiyo.
Kuna wageni ambao watafikia hotelini, kwenda uwanjani na kurejea makwao. Uzuri na umaridadi wa uwanja watakaouona siku hiyo, utabaki kuwa taswira ya kudumu kwao kuhusu nchi yetu. Kama wataamua kurejea tena Tanzania – kwa mazoezi au kwa mechi; kama ambavyo nchi nyingine jirani zimeomba kutumia uwanja wetu, siku hiyo moja inaweza kuwa siku yao ya kufanya uamuzi. Uwanja huu ni sawa na sebule ya taifa pale linapokuja suala la michezo.
Jicho la mbali
Tanzania imeomba kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda. Ukarabati huu wa sasa unaiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa na uwanja wenye vigezo vyote vinavyokubalika na CAF wakati nchi nyingine zikiwa zinajipanga. Hata kama ukarabati huu usingefanyika sasa, ungefanyika – pengine kwa gharama kubwa zaidi kwa serikali, kama sehemu ya kujiandaa na wenyeji wa AFCON.
Uzalendo kwa Taifa
Shilingi bilioni 31 zitakazotumika kukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa zitalinda heshima ya taifa letu. Taa za Uwanja wa Mkapa zinapozimika mbele ya wageni wa kitaifa, Wimbo wa Taifa unapogoma kucheza kwenye mashindano, luninga ya matokeo inapozima wakati mechi zikiendelea, aibu inakuwa ni kwa taifa zima na si walio uwanjani pekee.
Shilingi bilioni 31 ni pungufu ya fedha ambazo nahodha wa zamani wa Liverpool, Jordan Henderson, ataenda kulipwa na timu yake mpya ya Al Ettifaq ya Saudi Arabia. Katika mwezi na wiki ambayo tunaadhimisha miaka mitatu tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyefanya jitihada kubwa kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwanja wenye hadhi ya kimataifa, ni muhimu kubeba jukumu la kizalendo la kuhakikisha mojawapo ya alama za nchi inabaki katika hali nzuri wakati wote.
Ni mawazo yangu kuwa wadau wa michezo wamekuwa na kauli za kukanganya kuhusu masuala ya maendeleo ya mpira wetu. Zinapotokea changamoto za kuaibisha uwanjani, lawama hutolewa kwa wahusika lakini yanapotoka maamuzi ya kufanyia kazi changamoto hizo, zinakuja lawama kuwa gharama ni kubwa.
Taratibu, tunajenga utamaduni wa “ukifanya unakosea, usipofanya unakosea”. Huu ni utamaduni wa hatari.
Mwisho
0 Comments