Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesisitiza umuhimu wa tahadhari na uangalifu katika matumizi ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi.
Msisitizo huo umetolewa na Mkuu wa Huduma kwa Wateja TCRA, Thadayo Ringo, wakati wa uhamasishaji wa umma katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya 47 yaliyoendelea katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Alisema mamlaka hiyo inatoa elimu kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano katika sekta ya simu, mtandao, utangazaji na posta.
Ringo, alisisitiza umuhimu wa watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kuchukua tahadhari wakati wote wanapotumia huduma hizo.
Aliwasihi watumiaji kutowapa ushirikiano wadanganyifu wa mtandaoni wanaowalaghai ili wasalie kuwa salama wakati wote wanapotumia huduma za mawasiliano.
“Kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, nawashauri kuacha kutoa ushirikiano kwa wahalifu wa Mtandao wanaowapigia simu na kuwadai malipo kwa huduma zisizojulikana, mtu akijaribu kukulaghai mripoti kwa kutuma ujumbe wake au namba yake kwenda 15040” alisisitiza.
Alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa haraka iwezekanavyo wakati wanapobaini simu za udanganyifu kupitia namba 15040.
Aidha, aliwahimiza watumiaji kuwa macho dhidi ya ujumbe mfupi wa udanganyifu, “kama vile 'ile hela tuma kwenye namba hii; usipige spika mbovu” akiwasisitiza watumiaji huduma za mawasiliano kuwaripoti wahusika kwenda namba 15040.
Aliwahimiza Watoa Huduma za mawasiliano na wawekezaji wanaotarajia kuingia katika sekta hiyo, kutumia "Tanzanite Portal" ya TCRA ambao ni mfumo bora wa maombi ya leseni.
Alielezea kuwa portal hiyo, inayopatikana kupitia kwa www.tanzanite.tcra.go.tz inawawezesha watoa huduma kupakia maombi, kuhuisha leseni na kupokea mrejesho kuhusu huduma zao, bila kutembelea ofisi za TCRA.
“Maendeleo haya yanasaidia kuwezesha mchakato wa utawala na kurahisisha mawasiliano kati ya TCRA na wadau,” alisema.
Ringo aliwashauri watu binafsi ambao wanapoteza vifaa vya mawasiliano kuripoti haraka matukio hayo kwenye kituo cha polisi kilicho karibu na utoa maelezo muhimu ya utambulisho, kama vile Nambari ya Kimataifa ya Vifaa vya Simu (IMEI) kwa simu za mkononi, kwani polisi wanaweza kusaidia kwa ufanisi katika kushughulikia kesi za wizi.
Aliwataka wananchi kuwasiliana moja kwa moja na watoa huduma, pale wanapokabiliwa na changamoto yoyote katika huduma za mawasiliano.
“Kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwasiliana na muhudumu wako. Sisi katika Idara ya Huduma kwa Wateja TCRA tunahakikisha kuwa wateja wanahudumiwa kulingana na maelezo ya masuala yasiyokamilika kutoka kwa mhudumu wa huduma.
Hapa ndipo tunapojenga daraja kati ya mtumiaji wa huduma kupitia mifumo iliyoanzishwa, ikiwa ni pamoja na kamati rasmi ya malalamiko,” aliongeza.
Ringo alisisitiza kuwa, mamlaka hiyo imeanzisha mfumo imara wa kupokea maoni kutoka kwa wadau wa mawasiliano.
Alisema mfumo huo huhakikisha kuna ushirikiano na majibu yanayofaa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wakati pia kuzingatia maslahi ya wadau wote, ambao ni pamoja na watumiaji na watoa huduma.
Wadau wa mawasiliano wanagawanywa katika makundi ya watumiaji na wateja.
Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Mhandisi Othman Sharif Khatib, alielezea azma ya TCRA ya kutekeleza kikamilifu malengo yake ya mpango mkakati ambayo ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau ili kuwafahamisha juu ya haki na wajibu.
“Tunaamini kwa dhati kwamba kuongeza uelewa ni muhimu katika kuboresha jukumu letu la usimamizi wa sekta kwa huduma tunazosimamia,” alisisitiza.
0 Comments