· Yasisitiza ‘usalama kwa wakazi Jirani na minara’ upo
Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekamilisha zoezi la upimaji wa kiwango cha mionzi ya masafa ya redio na simu katika mikoa kumi na tano (15) nchini, lengo likiwa ni kuwalinda watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi wanaoishi karibu na miundombinu ya minara ya Simu, Redio na Televisheni. Zoezi hili la upimaji lilitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Habari Maelezo mjini Dodoma.
“Upimaji wa kiwango cha mionzi itokanayo na minara na vifaa vya mawasiliano (Radio Frequency Electro Magnetic Field radiations - EMF) ulitekelezwa kwa umakini mkubwa katika bendi mbalimbali zinazotumika kutoa huduma za mawasiliano ya simu, redio, na televisheni,” alisisitiza Dr Jabiri.
Alisema matokeo ya upimaji huo yanaonyesha kuwa kiwango cha mionzi katika maeneo yote yaliyopimwa kipo chini ya viwango vinavyokubalika na vilivyoelekezwa na International Commission on Non-Ionizing Radiation Protection (ICNIRP).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dk. Jabiri Bakari, kiwango cha juu cha mionzi kilichopimwa katika bendi ya FM Radio (87.5- 108 MHZ) kilikuwa ni 4.986 V/m (Volt per Meter), ambacho kipo chini sana ya kiwango cha juu kinachoelekezwa na ICNIRP ambacho ni 27.7 V/m. Vivyo hivyo, katika bandi ya matangazo ya televisheni (TV UHF (DTT) - 470 – 694 MHZ), kiwango kilikuwa 4.928 V/m (Volt per Meter), ambacho ni chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP ambacho ni 29.8 V/m.
Kwa upande wa huduma za data LTE, kiwango cha mionzi katika Digital Dividend II (694 – 790 MHZ) kilikuwa ni 3.823 V/m (Volt per Meter), ambacho ni chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP cha 36.2 V/m. Katika bandi ya Digital Dividend I (790 - 862 MHZ), kiwango cha mionzi kilikuwa ni 5.738 V/m (Volt per Meter), pia kipo chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP cha 38.6 V/m.
Aidha, katika bandi ya mawasiliano ya simu (GSM 900: 925 - 960 MHZ), kiwango cha mionzi kilikuwa 4.644 V/m (Volt per Meter), ambacho ni chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP cha 41.8 V/m. Vilevile, katika bandi ya mawasiliano ya simu (GSM 1800: 1805- 1880 MHZ), kiwango cha mionzi kilikuwa 4.659 V/m (Volt per Meter), ambacho pia ni chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP cha 58.4 V/m. Na mwisho, katika bandi ya mawasiliano ya simu na data (WCDMA/UMTS): 2110- 2170 MHZ), kiwango cha mionzi kilikuwa 6.807 V/m (Volt per Meter), na hata hiki kipo chini ya kiwango cha juu cha ICNIRP cha 63.2 V/m.
Kwa mujibu wa Dk. Jabiri Bakari, matokeo ya upimaji huo yanaonesha wazi kuwa kiwango cha mionzi kutoka kwenye minara ya huduma mbalimbali za mawasiliano hakijavuka viwango vinavyokubalika na ICNIRP, na hivyo kuwa salama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini. Hivyo, wananchi wanaweza kuwa na uhakika wa usalama wao wanapotumia huduma za mawasiliano ya simu, redio, na televisheni katika maeneo yao.
Dk. Jabiri Bakari ametoa wito kwa umma kutokuwa na wasiwasi, kwani TCRA itaendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa viwango vya mionzi vinabaki ndani ya mipaka ya usalama iliyowekwa na wataalamu wa kimataifa. Hatua hii ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na kuimarisha matumizi salama ya teknolojia ya mawasiliano.
Katika Mkutano huo na wanahabari ambao huratibiwa na Idara ya Habari Maelezo ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari TCRA iliahidi kuendelea kufanya tafiti na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miundombinu ya mawasiliano nchini inazingatia viwango vya kimataifa vya usalama. Wananchi pia wametakiwa kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika kwa kutoa taarifa pale wanapoona dalili za kutofuatwa kwa viwango vya mionzi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
***
0 Comments