Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YADHAMIRIA KUTOA MAFUNZO YA AMALI, VETA 65 KUJENGWA NCHINI

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia imekiri kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha inakidhi matarajio ya wananchi kwa kujenga Vyuo 65 vya Ufundi Stadi (VETA) nchini, vikiwemo 64 vya Wilaya na kimoja cha Mkoa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Adolf Mkenda ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Tanga, akiwa katika chuo cha Veta mkoani humo ambapo alieleza malengo ya serikali kuhusu ujenzi wa vyuo hivyo.


Waziri Mkenda amebainisha kwamba amefurahishwa na uongozi wa chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 mpaka sasa kimejenga mahusiano mazuri na viwanda kwa ajili ya kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji maalumu, kama vile ufundi bomba wanafunzi wanapelekwa kufanya kazi kwa vitendo wakishirikiana na mafundi kwa ajili ya kupata uzoefu kazini.


"Lakini kwa ujumla wake, serikali inawekeza sana katika ujenzi wa Veta, na sasa hivi tunajenga Veta 65, ambapo 64 ni za Wilayani na moja ya Mkoa, na kila mahali ambapo Veta inajengwa watu wana matumaini makubwa sana, hata tukiwa Bungeni maswali mengi yanayoulizwa katika Wizara yetu ni Veta" amesema.


"Kwa maana hiyo sisi tuna kazi ya kuhakikisha tunakidhi matarajio yao kwa kutoa elimu ya amali ambayo ni bora na inayokidhi matakwa, kikubwa ni kuwapima wahitimu wetu" amebainisha Waziri Mkenda.


Hata hivyo amefafanua kwamba, pamoja na mazuri yanayofanywa na baadhi ya Veta nchini, bado kuna mapungufu katika baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa maboresho ili hata wahitimu wakimaliza waweze kupata ajira kwa haraka na sehemu zenye viwango.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Antoni Kasore amesema ujio wa Waziri katika chuo hicho ni kujionea namna wanavyotoa mafunzo lakini pia huduma kwa wananchi ambapo ametoa maenelekezo ambayo tutakwenda kutafanyia kazi.


"Maelekezo yake ni kuwa tuweze kujitazama katika maeneo yetu ya ndani ya uzalishaji, kwahiyo ni lazima twende tukajitazame, tukajipime na kuweka mipqngo na mikakati ili mwisho wa siku tuhakikishe tunaenda kutoa huduma ambayo itatupatia mapato yatayoweza kuendesha shuhuli zetu" amesema.


"Lakini pia tutaweza kwenda kutoa huduma zinazokuwa zinahitajika kwa wananchi, hususani kwenye hoteli na kumbi za mikutano, lakini pia tutakwenda kutoa mafunzo bora ili kuwafanya wananchi waridhike na elimu ya ufundi stadi, kwahiyo tunamuahidi muheshimiwa Waziri kwamba tutakwenda kutekeleza agizo lake" amesisitiza.
Waziri Mkenda akipandq mti katika moja ya kiwanja kilichopo chuo cha VETA jijini Tanga ishara ya kumbukumbu ya kutembelea chuoni hapo.

Post a Comment

0 Comments