Ticker

6/recent/ticker-posts

ROYAL TOUR, REGROW VYAPAISHA UTALII WA KUSINI



Na John Mapepele

Hifadhi ya Taifa Mikumi imeanza kupokea mafuriko ya watalii wa ndani na nje ya nchi, kutokana matokeo chanya ya Filamu ya The Royal Tour na maboresho makubwa ya miundombinu inayowezesha ndege kubwa kutua na kuondoka kwa usalama misimu yote yaliyofanywa na Serikali kupitia Mradi wa Kukuza na Kuendeleza Utalii Kusini mwa Tanzania REGROW.

Wadau mbalimbali waliofurika kutembelea Hifadhi hiyo leo wamepongeza jitihada za Serikali za kufanya maboresho makubwa katika kipindi hiki chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Sulihu Hassan ambapo wamefafanua kuwa barabara za hifadhi zinapitika hata na magari madogo katika kipindi chote cha mwaka.

“Nampongeza Rais wetu kwa maono yake ya kuongoza kucheza Filamu ya Royal Tour na uongozi wa Wizara ya Maliasili chini Mhe. Mchengerwa wamefanya mapinduzi makubwa katika kipindi kifupi na matokeo tunayaona wageni wamefurika hata sisi wageni wa ndani tunaweza kuja na magari yetu madogo na kufanya utalii hapa mikumi bila shida yoyote kwa kipindi chote cha mwaka mzima” amesema mgeni, Moses Ibrahimu aliyekutwa hifadhini

Rubani wa ndege ya Flightlink, Bw. Khalid Amarjit, amesema amepongeza maboresho makubwa katika Hifadhi hiyo, ambayo amesema kuboreshwa kwa viwanja vya ndege katika hifadhi hiyo kunawarahisishia kutua na kuruka kwa uhakika.

Bi. Lee Gad,mtalii kutoka nchini Israel amesema baada ya Utalii visiwani Zanzibar ameshawishika kutembelea Hifadhi ya Mikumi ili kujionea Utajiri Mkubwa wa Wanyamapori na Mimea uliopo nchini kwani kwa muda mfupi utaweza kuona Simba, Chui, Tembo, Twiga na wengineo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amefafanua kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kuboresha miundombinu yote ya utalii katika hifadhi zote nchini ili wageni waweze kutembelea maeneo hayo na kupata huduma za kisasa.

"Nisema tu kwamba watanzania wategemee maboresho makubwa katika maeneo yetu hususan maeneo ya kusini mwa Tanzania kupitia mradi wa REGROW ili kuongeza maeneo ya wageni kuja kutembelea katika nchi yetu badala ya kutegemea maeneo machache kwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya vivutio nchi nzima."Amesisitiza Mhe Mchengerwa

Akizungumzia juu ya ongezeko kubwa la watalii, Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi Ignance Gara, amesema Hifadhi imekuwa ikipokea wageni wengi katika kipindi hiki tofauti na kipindi cha nyuma ambapo amesema hifadhi imejipanga vizuri kuwapokea na ametoa wito kwa watanzania wote kutembelea hifadhi hiyo yenye vivutio vya kipekee.

Post a Comment

0 Comments