Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Araman Benoite, amesema kaampuni hiyo imegawa bure mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa mamalishe wilayani Ilemela, kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Oryx Gas imegawa mitungi na majiko hayo jana kwa wanawake wajasiriamali wa Mama Lishe waliopo katika Kata 19 za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, kuwaongezea nguvu katika shughuli zao na kuzifanya kisasa.
Akizungumza mbele ya viongozi wa Wilaya ya Ilemela wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angelina Mabulla, Benoite amesema kuwa wameendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda na kutunza mazingira kwa kuhamasisha nishati safi ya kupikia.
“Katika mwendelezo huo wa kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama kwa kupikia, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited imekuwa mstari wa mbele kufikia azma hiyo, leo (jana) kampuni yetu imevitupia macho vikundi vya wafanyabiashara wa vyakula (Mama Lishe) wilayani Ilemela kwa kuwakabidhi bure mitungi 500 ikiwa na gesi yake.
“Utoaji huu wa mitungi ya Oryx umefanikiwa kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Waziri wa Dk. Mabula. Malengo ya kampuni ni kuona mabadiliko katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa jamii zote za Watanzania,” amesema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inaendana na mpango wa serikali wa miaka 10 wa matumizi salama ya nishati safi ya kupikia huku akifafanua wanafahamu kundi la Mama Lishe kila siku linahudumia chakula kwa wananchi lakini wengi wao wameathirika kwa namna mbalimbali kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.
“Mwanza na mikoa ya Kanda ya ziwa imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na ukataji miti kwa matumizi ya kuqndaa chakula, hivyo juhudi kubwa inahitajika kulinda afya na kuokoa mazingira ya ukanda huu na maeneo mengine nchini,” Amesema.
Aliongeza Oryx Gas inawekeza katika siku zijazo kwa kutekeleza mipango ya kukabiliana na kaboni kupitia elimu ya upishi safi, uchangiaji wa vifaa vya kuanzisha LPG bila malipo kwa baadhi ya mikoa, uhamasishaji wa matumizi ya LPG kupitia uuzaji mkubwa wa mitungi ya gesi kwa bei nafuu.
WAZIRI DK. MABULA APONGEZA
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabulla amesema hatua ya Kampuni ya Oryx Gas kutoa hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono kwa inaisadia serikali kuhanasisha utunzaji mazingira nchini
Dk. Mabula akizungumza katika hafla ya kukabidhi majiko hayo, Ilemela jijini Mwanza, Waziri Dk. Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela amesema yatagawanywa katika kata zote 19 za wilaya hiyo kulingana na shughuli zinazofanywa na Mamalishe wilayani humo.
“Tunaona namna ambavyo akinamama wanapata shida katika kutekeleza shughuli zao kwa haraka, katika mazingira mazuri, lakini tunahitaji kutunza mazingira yetu. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha huduma zote anazotoa kaanzia kwenye huduma za uchumi, kaja kwenye elimu lakini uwekezaji ameupa kipaumbele.
“Ukija katika huduma za jamii akina mama wengi wamekuwa wakihanagika kutafuta kuni na mkaa, wanakwenda kufyeka misitu.Tumetajiwa hadi kiwango cha uharibifu ambacho kimefanyika. Sasa tunapopata kampuni kama hizi ambazo ziko tayari kuwekeza katika afya na utunzaji bora wa mazingira yetu, lazima tuwashukuru,” ameema.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akitoa elimu ya matumizi salama ya mtungi wa gesi ya Oryx kabla ya mitungi hiyo kukabidhiwa kwa wanawake wajasiriamali wilayani Ilemela mkoani Mwanza
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Araman Benoite.
Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite akizungumza wakati wa tukio la ugawaji mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Mama Lishe waliopo katika Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
0 Comments