Ticker

6/recent/ticker-posts

MKOMBOZI BENKI YAPUNGUZA KIASI CHA HASARA LIMBIKIZi KUTOKA SH.BIL 11.3 HADI SH.BIL 1.49

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Benki ya Biashara Mkombozi ilitangaza faida baada ya kodi ya Sh. 6.79billioni kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi za fedha kwa mwaka 2022. Hii ni matokeo ya juhudi mbalimbali za kuongeza mapato na kuleta ufanisi katika utendaji wa Benki kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo Julai 29,2023 Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara Mkombozi Bw. Respige Kimati katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kumi na Nne wa wanahisa wa Benki ya Biashara ya Mkombozi uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Mkurugunzi Mkuu alisema; Benki iliendelea kustahimili changamoto mbalimbali na kuonesha matokeo mazuri sambamba na vipaumbele vya kimkakati, kuboresha ufanisi na ubora wa mikopo, kuimarisha mizania na kuvuna mapato mazuri. Hii ni baada ya kujenga msingi imara kupitia utekelezaji wa mkakati wetu wa “Mageuzi na Maboresho” (2020-2023), tuliongeza kasi ya utekelezaji ili kuimarisha mafanikio tuliyoyapata na kuwasilisha malengo muhimu ya mwaka 2022

Tumepiga hatua nzuri katika safari yetu ya mabadiliko kimkakati na matokeo yake yako wazi. Haya ni matokeo ya miaka mingi ya uthabiti na nidhamu katika usimamizi wa gharama, maboresho ya mikopo, mpangilio wa huduma na mchakato pamoja na uwekezaji kwa rasilimali watu na teknolojia.

Tumekuwa na ufanisi zaidi. Tumeshughulikia changamoto za mikopo na utendaji wa zamani. Tumeimarisha mtaji na kutoa huduma nyingi zaidi kwa njia za kidijitali. Matokeo ya haya yote ni Benki kupata ongezeko kubwa zaidi la faida ambayo haijawahi kutokea katika historia yake. Wanahisa wanao mchango mkubwa sana katika mafanikio haya kwa sababu ndiyo waliojitolea katika safari ya kuongeza mtaji wa Benki. Kwa miaka mitatu iliyopita,

Benki imepunguza kiasi cha hasara limbikizi kutoka Shilingi bilioni 11.3 mwaka 2019 hadi Shilingi bilioni 1.49 hivi sasa. Fedha hizi zimesaidia sana kuongeza mtaji wa Benki. Ni matarajio yetu kwamba tutaukamilisha mkakati wetu mwaka 2023, na kuanza kupata faida limbikizi, hatua itakayotuwezesha kujenga uwezo wa kutoa gawio kwa wanahisa wetu.

Jambo hili ni muhimu wakati huu tunapotafuta mbinu za kupanua vyanzo vyetu vya mapato ili kuchochea ongezeko la faida na azma yetu ya kuikuza zaidi Benki". Ameongeza Kimati.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Bw.Gasper Njuu amesema Benki hiyo imekamilisha mchakato wa kutengamanisha huduma zao na zile za wadau wengine muhimu katika utoaji wa huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali kama vile kampuni za simu za mkononi na wengine.

Amesema wamepata mafanikio mazuri katika mchakato wa kuanzisha na kufikisha huduma kwa njia ya Mawakala wa Benki (Mkombozi WAKALA), Kukusanya sadaka kwa njia ya kidijitali (SADAKA Digital) na kutoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao (Internet Banking).

"Pamoja na mafanikio hayo pia Tumeimarisha chaneli yetu ya benki kwa njia ya Simu (Mobile Banking Channel) kwa kuzindua programu ya App. Wakati huohuo, wateja wetu wakipata huduma zetu kwa njia ya USSD". Amesema

Pamoja na hayo amesema wamekamilisha mipango ya kufungua matawi mapya Arusha na Mwanza ambayo yataanza kufanya kazi kabla ya mwisho wa robo tatu ya mwaka 2023. Tawi la Arusha lilifunguliwa na kuanza kutoa huduma tarehe 24 Mei, 2023.

Aidha amesema kuwa kwa ujumla, mipango yao ya uimarishaji wa biashara na matarajio ya ukuaji wake yanaendelea kuleta matokeo chanya katika kuongezeka kwa idadi ya wateja, kuongezeka kwa mapato, usimamizi bora wa gharama za matumizi na ubora wa usimamizi wa vihatarishia hatari.
Mwenyekiti wa bodi Bw. Gasper Njuu (kulia) akikabidhi kitabu cha Mkutano Mkuu wa 14 wa Wanahisa wa Benki ya Biashara Mkombozi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya (kushoto) ambaye ni Mkurugenzi wa Bodi ya Mkombozi wakati wa Mkutano huo.



Post a Comment

0 Comments