Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA WIKI YA MAADHIMISHO YA JKT

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuhakikisha wanafanya uwekezaji zaidi katika kufundisha vijana matumizi ya teknolojia katika shughuli zake mbalimbali za uzalishaji mali na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa na Maonesho ya JKT yanayofanyika katika Viwanja vya Suma JKT House eneo la Medeli Mashariki Jijini Dodoma.

Amesema ulimwengu wa sasa ni wakutumia teknolojia na akili zaidi kwa kuwa matumizi ya teknolojia yamedhihirisha uwezo mkubwa wa kuwezesha na kurahisisha utendaji kazi katika nyanja mbalimbali.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa Rai kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuona umuhimu wa kuwatambua wataalam wake wabunifuni na kuwapa tuzo sambamba na kushirikiana na Taasisi husika kuwa na haki miliki ya ubunifu na gunduzi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi hilo.

Makamu wa Rais amesema katika kutekeleza dhima ya kuwaandaa vijana wa Tanzania ili kuwajengea nidhamu, uzalendo, ukakamavu na kuwafundisha ujuzi na hatimaye kuchangia katika ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi, hapana budi kuweka mkazo katika suala la ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Amesema juhudi za kupanda miti na uhifadhi wa mazingira zifanywe na Kambi zote za JKT nchini, ili kuhakisha mazingira yanatunzwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia amesisitiza juu ya matumizi ya nishati safi ili kupunguza ukataji miti ovyo pamoja na kutoa msisitizo kwa JKT kuunga mkono udhibiti wa taka za plastiki, kwani huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuhakikisha wanashirikiana na Taasisi zingine katika kutafuta suluhisho la upatikanaji wa chakula cha samaki hapa nchini.

Pia amesisitiza taasisi za kifedha ikiwemo Mabenki kutoa elimu kwa Vijana wa JKT na kuwawezesha upatikanaji wa mikopo ili waweze kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika wiki nzima ya maadhimisho ya miaka 60 ya JKT ili kuweza kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa pamoja na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na utengenezaji bidhaa.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema Wizara itaendelea kuijengea JKT uwezo ili kuweza kuongeza uzalishaji wake kupitia Suma JKT na kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.

Amesema kwa kushirikiana na Wizara zingine za kisekta wanatarajia kuboresha mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wa JKT na kuwawezesha kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ili baada ya kuhitimu waweze kujitegemea kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Waziri Bashungwa ameongeza kwamba pamoja na malezi kwa vijana JKT inapaswa kuwa na ubunifu na kutoa mchango kwa taifa, kuzalisha ajira na kulisaidia taifa kuwa na chakula toshelevu.

Awali akitoa taarifa juu ya Maendeleo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema licha ya changamoto mbalimbali JKT imefanikiwa kufikia dhumuni la kuanzishwa kwake kwa kutoa mafunzo ya malezi kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujitegemea na kuleta maendeleo endelevu na utangamano wa kitaifa.

Amesema malengo hayo yametekelezwa kwa ufanisi na kufanikiwa kuwabadili vijana kifikra, kuwajenga katika hali ya umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu, uzalendo na uelewano bila kubaguana kwa misingi ya ukabila, udini, jinsia na kudumisha uhuru na amani ya Taifa.

Meja Jenerali Mabele ameishukuru serikali kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za Jeshi hilo ikiwemo kuendelea kutenga fedha ili kuboresha miundombinu itakayowezesha kuchukua vijana wengi zaidi kwaajili ya mafunzo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mstafeli katika eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Chamwino mkoani Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mnara wa Miaka 60 ya JKT uliopo katika eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Chamwino mkoani Dodoma. Uzinduzi huo ni katika Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023. (Wengine katika Picha ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vita Kawawa)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizindua Mnara wa Miaka 60 ya JKT uliopo katika eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Chamwino mkoani Dodoma. Uzinduzi huo ni katika Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023. (Wengine katika Picha ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vita Kawawa)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na Jeshi la Kujenga Taifa na Wadau wengine kutoka nje ya JKT yaliopo katika viwanja vya Suma JKT House eneo la Medeli Mashariki Jijini Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwapa Samaki chakula katika moja ya Bwawa la kufugia Samaki lilibuniwa na Jeshi la Kujenga Taifa wakati akitembelea maonesho ya Miaka 60 ya JKT yanayofanyika katika viwanja vya Suma JKT House eneo la Medeli Mashariki Jijini Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na JKT na Wadau wengine kutoka nje ya JKT katika viwanja vya Suma JKT House eneo la Medeli Mashariki Jijini Dodoma leo tarehe 01 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipokea zawadi tuzo kutoka kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa mara baada ya Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT iliofanyika mkoani Dodoma leo tarehe 01 Julai 2023.

Post a Comment

0 Comments