Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WANANCHI Mkoa wa Tanga wameombwa kuendelea kudumisha amani na utulivu na kuacha kuwasikiliza na kukubali maneno ya uchonganishi yanaoenezwa na vyama vya siasa vya upinzani kwa lengo la kuiponda serikali.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) Mkoa wa Tanga Rajabu Abdalla ametoa rai hiyo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Msambweni, jijini Tanga ambapo alisema lengo la mkutano huo ni kuimarisha chama kwa ajili ya chaguzi mbalimbali zijazo.
Amesema suala zima la amani, utulivu na maendeleo vilivyopo mkoani humo na nchi kwa ujumla vinapaswa kulindwa kwani ni muhimu katika Taifa na ni matokeo makubwa yaliyoenziwa ndani ya serikali ya Ccm, hivyo kukataa mawazo ya kupotosha yanayoendelea kuenezwa na wapinzani.
"Tabia ya mwanadamu, jambo ambalo amezoea kuishi nalo huwa analiona ni la kawaida sana, lakini ikitokea siku analikosa ndio ataelewa kumbe lilikuwa na umuhimu na siyo kawaida, kwakuwa tumezoea kuishi kwa amani na utulivu ndani ya nchi yetu tunaona vya kawaida,
"Ukiona amani na utulivu vibaendelea kudumu katika nchi yetu havijaja kwa bahati mbaya bali ni mikakati na nia ya makusudi ya chama cha mapinduzi, kwahiyo mnapoona vinadumu mjue ni sera madhubuti ya chama chetu" amesisitiza.
Aidha amebainisha kwamba maneno na vitendo vya wapinzani vinaonesha viashiria vya wazi vya uvunjifu wa amani na utulivu na ndiomaana hata wakisimama kwenye majukwaa yao hawahutumii sera waliyonayo bali wanaishia kutoa maneno yasiyofaa ya matusi na kejeli kwa viongozi wa Ccm.
"Wenzetu hawa kwa maneno na vitendo vyao tuu vinaashiria tukiwapa nchi na kushika dola, naamini amani na utulivu wa nchi yetu vitapotea mchana kweupe, sisi wanaCcm hatukuzoea matusi wala kukejeli mtu na hatuthubutu maana hatukulelewa hivyo",
"Ccm tuna maneno na matendo mengi mazuri ya kuwaambia wapinzani wetu na siyo matusi au kejeli lakini pia hatutakiwa kufanya hivyo kwao bali kuwaonesha busara ili waweze kuja kujiunga na chama chetu" alibainisha mwenyekiti.
"Rais wetu anatumia busara na hekima kuendelea kuilinda amani ya nchi yetu, lakini wenzetu wanatumia nguvu kubwa kuivunja, tunachowaambia wananchi kwamba jambo hili tusilikubali, wakataeni zaidi ya tunavyoukataa ukoma" amesisitiza.
Hata hivyo mwenyekiti amefafanua kwamba serikali imefanya mengi katika Mkoa wa Tanga ndani ya kipindi cha miezi sita katika suala zima la huduma za jamii katika sekta za maji, elimu, afya na pia miundombinu jambo ambalo linaleta matumaini kwa wananchi na serikali yao ya awamu ya sita.
Amesema kwa upande wa miradi ya maendeleo, serikali imeingiza zaidi ya sh B. 356 katika ujenzi wa shule, miundombinu, vituo vya afya, zahanati na hospitali katika Mkoa, "ndani ya kipindi cha miezi sita, Mh. Rais Samia Suluhu Hassan ametuingizia zaidi ya sh B. 5 lakini pia kwa upande wa maji ametupa zaidi sh B. 27" amesema.
Pia amebainisha kuwa kwenye mradi wa maji wilayani Mkinga wamepokea zaidi ya sh B. 35 huku mradi wa kutoka Segera hadi Kabuku wilayani Handeni wamepokea zaidi ya sh B. 25.
"Lakini Mh. Rais alipanga kumaliza kabisa tatizo la maji katika miji 28 nchini, na Mkoa wa Tanga tumepewa miji minne ambayo ni Pangani, Muheza, Korogwe na Handeni na ametupa sh B 181 na hivi sasa Mkandarasi yupo eneo la tukio" amesema.
0 Comments