Ticker

6/recent/ticker-posts

MAAGIZO YA RAIS SAMIA YASHUSHA BEI YA MAFUTA TANZANIA

* Kenya bei ya mafuta yazidi kupaa, wenye magari wavuka mpaka hadi Tanzania kuweka mafuta

* Maagizo ya Rais Samia ya usimamizi wa uingizaji mafuta nchini na ruzuku yaleta ahueni kwa Watanzania


Mwandishi Wetu Dar es salaam

MAAGIZO ya Rais Samia Suluhu Hassan yamesaidia kushusha bei ya mafuta ya petroli na dizeli nchini kwa mwezi wa pili mfululizo, huku nchi jirani ya Kenya wakilia na ukali wa maisha unaotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.


Baadhi ya wamiliki wa magari kutoka Kenya wameamua kuvuka mipaka hadi Tanzania ili kuweka petroli na dizeli kwenye vituo vya mafuta vya nchini Tanzania, ambavyo huuza mafuta kwa bei ya chini kuliko Kenya.


Takwimu za EWURA zinaonesha kuwa kwa mkoa wa Dar es Salaam, bei ya kikomo ya petroli mwezi wa Julai imeshuka kwa Shilingi 137 kwa lita hadi kufikia Shilingi 2,736, wakati bei ya dizeli imeshuka kwa Shilingi 118 kwa lita hadi kufikia Shilingi 2,544.


Kwa sarafu ya Kenya, bei ya mafuta Tanzania ni sawa na Shilingi za Kenya, Ksh 147.96 kwa lita ya dizeli, na Shilingi za Kenya Ksh 159.13 kwa lita ya petroli.


Wakati kwa upande wa nchini Kenya, bei halisi ya petroli ni Shilingi za Kenya Ksh195.53 kwa lita wakati bei ya dizeli ni Shilingi za Kenya Ksh179.67 kwa lita.


"Madereva wa magari wengi wa Kenya wanavuka mipaka ya Namanga na Sirari na kuja Tanzania kuweka mafuta ya petroli na dizeli kwenye vituo vya mafuta vya Tanzania kwa ajili ya unafuu wa bei," Aloyce Mushi, mfanyabiashara wa mafuta wa Arusha alisema.

Ahueni ya bei ya mafuta nchini Tanzania imetokana na maagizo mahsusi ya Rais Samia kuwa serikali yake ichukue hatua za kupunguza kupanda kwa gharama ya maisha nchini.


Rais Samia aliagiza kuwa serikali itoe ruzuku ya Shilingi Bilioni 100 kwenye bei ya mafuta kila mwezi ili kudhibiti kupanda kwa bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.


Rais Samia aliagiza pia kuwa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ihakikishe kuwa inadhibiti ushindani wa makampuni yanayoingiza mafuta nchini kwa lengo la kushusha bei.


Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) nalo limeingia kwenye biashara ya kuagiza mafuta kwa pamoja ili kuleta ushindani kwa kampuni binafsi na kuhakikisha bei ya mafuta inashuka nchini.


Ahueni ya bei ya mafuta nchini Tanzania imeleta manufaa kwenye uchumi na pia kushusha gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida.


Gharama za usafirishaji wa mizigo mbalimbali, ikiwemo chakula na bidhaa za nyumbani imeweza kudhibitiwa kutokana na bei ya mafuta kushuka.

Mafuta ya petroli na dizeli ni miongoni mwa bidhaa zinazochangia kupandisha au kushusha mfumuko wa bei nchini.


Mfumuko wa bei kwa mwezi Mei 2023 ulishuka hadi kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.3 kwa mwezi Aprili 2023, kwa mujibu wa takwimu za NBS.


Wakati huo huo, bomba la TAZAMA lililojengwa miaka ya 1960 ambalo lilikua linasafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania hadi Zambia, sasa litaanza kusafirisha mafuta ya dizeli kutoka Dar es Salaam hadi Zambia, badala ya mafuta ghafi kama ilivyokua hapo awali. 

Waziri wa Nishati, January Makamba, amesema kuwa baada ya kuanza kusafirisha dizeli kwenye bomba la mafuta, hali ya usalama na mahitaji ya usalama ya bomba hilo yameongezeka sababu ni rahisi watu kushawishika kutoboa bomba hilo na kuchukua dizeli.


"Tumeshafanya mkutano wa kwanza mwaka jana na tuliweka makubaliano ya kuweza kulilinda bomba hili lenye urefu wa kilomita 1,710 kutoka Kigamboni, Dar es salaam, hadi Indeni-Ndola, Zambia,” alisema.

Makamba alisema kuwa bomba hili limejengwa muda mrefu na lina kipenyo chembamba, wakati biashara ya mafuta imekua na mahitaji ya mafuta yamekua makubwa zaidi.

Alisema kuna haja ya kujenga bomba pana na jipya litakalosafirisha pia bidhaa nyingine zaidi ya dizeli. Serikali zote mbili zimekua zikiongea kuhusu biashara hii ya mafuta na pia ujenzi wa bomba jipya la gesi ili kuiuzia Zambia gesi.


“Haya ni mashirikiano mazuri kati ya nchi zetu hizi na pia ni mwendelezo wa mahusiano mema unaofanywa na viongozi wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia, kama yalivyoasisiwa na Viongozi wetu wa kwanza Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na hayati Kenneth Kaunda.”

Post a Comment

0 Comments