Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo ameiwakilisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango mjini Songea yenye kauli Mbiu isemayo, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ambapo imehudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb).
Mwaipopo amesema kuwa sisi kama OWMS tayari tupo kwenye mikoa kumi na saba ikiwemo mkoa huu wa Ruvuma ambapo leo tumeshuhudia tukio hili likizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na tunatarajia kushiriki kikamilifu katika siku tisa zijazo ambazo Kampeni hii itatekelezwa mkoani Ruvuma
Sisi tuna amini katika kauli mbiu ya Kampeni hii ambayo inasema, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,’” tunasema kwamba Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ni chachu na nguzo katika kuleta maendeleo nchini ili kuleta usawa na amani Tanzania
Mwaipopo amesema kuwa ushiriki wetu unahusisha uwepo wa banda la maonesho katika uwanja wa Majimaji ambapo Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ruvuma, Egidy Mkolwa watakuwa wakiwahudumia wananchi wa Ruvuma wenye matatizo ya kisheria na kuwasikiliza na kuwashauri nini cha kufanya na wapi pa kwenda ili waweze kutatua matatizo yao.
OWMS ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na tumeshiriki kikamilifu Kampeni hii ambayo inalenga kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia na nyinginezo tunatekeleza Kampeni hii ya miaka mitatu kwa kuhakikisha kwamba wananchi wanyonge wa Tanzania, watoto, wanawake, wale ambao hawana uwezo wa kupata msaada wakisheria kwa gharama nafuu wanahudumiwa kupitia Kampeni hii
Ofisi ya Wakili wa Serikali ina Ofisi zake kwenye mikoa kumi na saba nchini ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Ruvuma, Tanga, Arusha, Mwanza, Rukwa, Kagera, Mara, Tabora, Iringa, Morogoro, Mtwara, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Kigoma ambayo inahusika kwenye mnyororo wa utoaji haki nchini hivyo ushiriki wake kwenye maonesho hayo inaipa fursa OWMS kupata changamoto za wananchi, kuwaelimisha na kufanyia kazi malalamiko yanayohusu taasisi za Serikali.
Kampeni hiyo imeandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria na itafanyika kwa siku kumi mkoani Ruvuma na imeanza Machi, 2023.
Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mercy Kyamba akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipotembelea banda la Ofisi hiyo kabla hajazindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria mjini Songea. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wananchi kabla hajazindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria mjini Songea. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo (hawapo pichani)
Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ruvuma, Egidy Mkolwe (wa kwanza kulia) wakihudumia wananchi kwenye banda la Ofisi hiyo wakiwapatia elimu kuhusu masuala ya kisheria wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango mjini Songea
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo akimkabidhi Jarida la Wakili Mkuu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alipotembelea banda la maonesho la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria mjini Songea
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Hakimu Japhet Manyama akipata maelezo kutoka Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, James Kibamba kuhusu majukumu ya Ofisi hiyo alipotembelea banda la maonesho la Ofisi hiyo wakati wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyofanyika mjini Songea
Mwananchi akifurahia jambo kwenye banda la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kupatiwa elimu kuhusu masuala ya kisheria na Mawakili wa Serikali wa Ofisi hiyo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango mjini Songea
Wanachi wakimsikikiza kwa makini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip akihutubia wananchi hao kabla hajazindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria mjini Songea. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo (hayupo pichani)
0 Comments