Ticker

6/recent/ticker-posts

JINSI MFUMO WA USAJILI NA UGAWAJI WA MIRABAHA UNAVYOFANYA KAZI (WIPOCOS)

Aliyekuwa Naibu Katibu  Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, hivi sasa Katibu Mkuu wa wizara hiyo akikabidhi hundi ya mfano kwa mnufaika wa mgao wa mirabaha uliyotangazwa Januari 28,2022.

Na Philemon Kilaka

Mnamo Januari 28, 2022 Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ilifanya mgao wa 23 wa mirabaha kwa kazi za Muziki kwa kuzingatia matumizi ya kazi katika vyombo vya habari. Utaratibu wa kufanya mgao kwa kuzingatia matumizi ni wa kimataifa na unaleta maana ya mrabaha. Awali COSOTA imekuwa ikifanya migao ya mirabaha kulingana na kazi zilizosajiliwa.

Katika mgao huo kiasi cha Tshs.312,290,259 kiligawiwa kwa Wasanii 1,123 kutokana na matumizi ya kazi 5,924 kutoka vituo vya Redio vilivyowasilisha taarifa zake.

Hivyo katika kufanya mgao COSOTA inatumia Mfumo wa Usajili na Ugawaji wa Mirabaha unaoitwa WIPOCOS. Mfumo huo unamilikiwa na Shirika la Miliki Bunifu Dunia (WIPO) na unatumiwa na nchi mbalimbali duniani .

Mfumo huo wa kugawa mirabaha huingizwa kazi zote zilizotumika kwa lengo la kuweza kufanya mgao vizuri kutokana na matumizi ili kubainisha kiwango cha mgao kutokana na Hakimiliki na Hakishiriki.

Katika kufanya mgao wa mirabaha mfumo wa WIPOCOS unahitajika kuwepo kwa taarifa mbili za msingi ambazo ni kiasi cha fedha zilizokusanywa na taarifa ya matumizi ya kazi kutokana na muda husika wa makusanyo.

Hivyo taarifa hizo huingizwa kwenye mfumo wa WIPOCOS na kuchakatwa. Mfumo hutengeneza kiwango cha fedha ambacho huainishwa kama bei ambayo italipwa kwa matumizi ya kazi (unit rate). Kiwango hicho ndicho hutumika kujizidisha katika mfumo kulingana na idadi ya matumizi ya kazi.

Mfano iwapo mfumo umechakata na kupata bei ya matumizi kwa wimbo mmoja ni Tshs.10,000 na msanii mmoja ana kazi moja ambayo imetumika mara 100 kutoka katika taarifa zilizoingizwa kwenye mfumo. Mahesabu yake ya kuchakata matumizi hayo yatafanyika : 10,000(bei) X 100(matumizi) = 1,000,000 hivyo mrabaha wa mbunifu huyo utakuwa ni Tshs. 1,000,000 mgao huu utakuwa hivi kwa mbunifu ambaye anamiliki kazi hiyo kwa asilimia 100% na amesajili hivyo. Kama usajili ni asilimia 50% kwa 50% ina maana kila mmoja katika kazi hiyo atapata shilingi 500,000.

Kwa upande wa kazi ambayo haijasajiliwa mnufaika hupewa mgao wa 100% kutokana na kazi kuwa imeingizwa kwa jina la mtu mmoja kutokana na taarifa zilizopatikana, hali hii husababisha kupotea kwa haki za wabunifu wengine ambao wameshiriki kuandaa kazi hiyo ila mnufaika anapokuja kuchukua mrabaha wake, atahitajika kufanya usajili wa kazi hiyo ili kuweka taarifa hizo vizuri na kubainisha hakimiliki na hakishiriki katika kazi hiyo ili mgao ujao wenye hakishiriki waweze kunufaika.

Uwepo wa Kanzidata ya watu waliyosajili kazi huleta maana ya kuwa na usahihi wa wamiliki halali wa kazi zilizotumika na ushahidi wa wenye hakimiliki na hakishiriki.

Lakini pia unapogawa mirabaha kwa kazi kama ya Muziki kwa kutumia taarifa za matumizi kutoka katika vyombo vya habari (logsheets/playlist), na maeneo mengine yanayofanya maonesho kwa umma unakuwa na ushahidi au uhalisia wa matumizi ya kazi za kila mnufaika wa mrabaha.

Mfumo wa Ugawaji Mirabaha “WIPOCOS” baada ya zoezi la kuchakata mgao,

hutoa jina la mnufaika wa mrabaha, pamoja na kiasi kilichopatikana kutoka katika kila nyimbo iliyotumika kutokana na taarifa zilizoingizwa kwenye mfumo na jumla ya pesa anazopata pamoja na taarifa ya kituo kilichotumia kazi yake.

Hivyo, ili uweze kupata mirabaha lazima kazi iwe imetumika na jinsi kazi inavyotumika mara nyingi ndivyo kiwango cha pesa kinavyoongezeka.

Maeneo ambayo huhitajika kulipia leseni za matumizi ya kazi kama Muziki kwa ajili ya mirabaha ni maeneo ya biashara kama Vyombo vya Habari ,Baa, Kumbi za Starehe,Kumbi za Sherehe,Supermarket, Migahawa, Vyombo vya Usafiri nk.

Mgao wa mirabaha hufanyika kwa kazi zote zilizotumika nchini ikiwemo kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi .kwa mujibu wa taarifa za matumizi


Post a Comment

0 Comments