Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) pamoja na wahusika wengine kuweka mkakati wa kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka mataifa mengine kusoma katika chuo hicho.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) yaliofanyika katika viwanja vya chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam.
Amesema kwa kufanya hivyo kutaongeza wigo wa mwingiliano, kubadilishana uzoefu na kujifunza ikijumuisha uwezekano wa kubadilishana wafanyakazi kutoka vyuo vingine vya Ulinzi vya Kitaifa pamoja na Taasisi katika mafunzo maalum.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba uandikishaji wa idadi kubwa ya washiriki wa kozi hizo wenye uwezo mkubwa wa uongozi kutoka nchi nyingine utachangia katika kukuza viongozi rafiki wa Tanzania wa Nchi za nje.
Amesema wahitimu hao wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa wana nafasi kubwa ya kuwa Mabalozi wa kipekee wa Tanzania katika masuala ya utalii, utamaduni, lugha ya Kiswahili na rekodi ya nchi ya kudumisha amani na utulivu wa kijamii na kisiasa tangu uhuru mwaka 1961.
Amesema NDC inapaswa kuwa kitovu cha elimu ya usalama na masomo ya kimkakati ya kikanda.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kwa lengo la mwendelezo na maendeleo ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi upo umuhimu wa kuwatumia wahitimu wa chuo hicho.
Amesema kupitia uzoefu wa kimataifa inaonesha kwamba wanachuo huongeza thamani kubwa kwa Vyuo wanavyohitimu kwa kutoa ushuhuda wenye nguvu kwa niaba ya chuo na hivyo kufanya chuo kujulikana na kuvutia wengine.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wahitimu wa Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi na wahitimu waliopita awali, kuchukua jukumu la kuendelea kukitumikia chuo kwa uaminifu popote watakapokuwa kwa maendeleo bora ya chuo hicho.
Vile vile ametoa rai kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi kufanya utafiti wa kufuatilia maendeleo ya wahitimu popote pale wanapopangiwa hasa kuzingatia matokeo yao kulingana na elimu waliyoipata kupitia mafunzo chuoni hapo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema bado idadi ya wanawake wanaopata mafunzo katika chuo hicho ni ndogo hivyo amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa Makatibu Wakuu wa Wizara kuwahamasisha wanawake kujiunga na kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema Chuo hicho kinawaandaa wahitimu namna mpya ya kufikiri na kukabiliana na changamoto za kiusalama zaidi kwa kutumia akili kuliko silaha.
Amesema changamoto za kiusalama na matishio mbalimbali katika nchi, bara la Afrika na duniani kwa ujumla yanatihaji kufikiri kwa kina na kuwa na maamuzi sahihi kwa kutoa suluhu zitazodumu kwa muda mrefu.
Meja Jenerali Mhina ameongeza kwamba mafunzo hayo yanatoa fursa kwa washiriki kukutana na viongozi wa juu kutoka serikalni, sekta binafsi na wataalamu mbalimbali ili kuelewa masuala ya kisiasa, kijamii na mikakati katika nchi husika.
Amesema NDC inahakikisha wahithimu wanafikiri vizuri na kufikiri nje ya mipaka ili kupata suluhu za muda mrefu katika matatizo yanayojitokeza na yale yasiotarajiwa kwa wakati huo.
Katika mahafali hayo washiriki saba (7) wamefanikiwa kufuzu Stashahada ya Usalama na Stratejia huku jumla ya washiriki thelathini na tatu (33) wakifanikiwa kufuzu Shahada ya Uzamili ya Usalama na Stratejia.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
29 Julai 2023
Kunduchi – Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwakabidhi vyeti Wahitimu wakati wa Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu mara baada ya kumalizika kwa Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023. (Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha NDC Balozi Moses Kusiluka, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Stergomena Tax, Mkuu wa Chuo cha NDC Meja Jenerali Ibrahim Mhona, Kansela wa Chuo cha NDC Dkt. Abdulhamid Mzee, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraj Mnyepe)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi mbalimbali, Wakufunzi pamoja na Wahitimu wakati wa Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Viongozi pamoja Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi katika maandamano wakati wa Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa ameongozana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda (Kulia) pamoja na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Meja Jenerali Ibrahim Mhona (kushoto) wakati alipowasili kushiriki Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Meja Jenerali Ibrahim Mhona wakati alipowasili kushiriki Mahafali ya Kozi ya 11 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) yaliofanyika katika chuo hicho kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Julai 2023.
0 Comments