Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi kupuuza hoja za baadhi ya watu wenye nia ovu wanaosema kwamba Serikali inampango wa kuuza Bandari ya Dar es Salaam huku wakijua fika kuwa ni mashirikiano ya kibiashara yanayofanywa na si vinginevyo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 14, Julai 2023 wakati wa mkutano wa hadhara alioufanya katika Kata ya Iyunga Jijini humo kwa lengo la kuwaelezea Wananchi baadhi ya ahadi alizozitekeleza katika Jimbo hilo ikiwemo Kata hiyo pamoja na yale yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Amewaeleza kuwa katika kipindi chake cha Uongozi wa miaka miwili ndani ya Jimbo hilo kwa kushirikiana na Serikali wameweza kufanikisha utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo kuwezesha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Inyala hadi Airport ambao utekelezaji wake umeshaanza.
Kuhusu changamoto ya maji na afya, Dkt. Tulia amewaeleza Wananchi hao kwamba Serikali imewezesha kupatikana kwa ufumbuzi huo kupitia mradi wa mto Kiwila ambao utamaliza tatizo hilo kwa Mkoa mzima wa Mbeya na kuhusu afya tayari Serikali imewezesha upatikanaji wa vifaa tiba katika Hospitali zote ndani ya Jiji hilo.
“Niwaombe sana, watu hawa wapuuzwe na niwahakikishie tupo salama na hakuna cha bandari wala nchi inayouzwa na hata wakija hao wanaosema imeuzwa waambieni wawapatie mgao wa hayo mauzo” Amesisitiza Dkt. Tulia.
0 Comments