Ticker

6/recent/ticker-posts

CCM KILOMBERO YAPONGEZA UREJESHAJI USHOROBA ZA TEMBO


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Mohamed Msuya akizungumza mbele ya wanachama wa chama hicho.

*********************

Na Selemani Msuya

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kimesema uamuzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) kurejesha Shoroba ya Tembo Kilombero ambayo inaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere utaleta afya kwa chama hicho.

STEP wanashirikiana wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tuhifadhi Maliasili ambalo limewezesha waandishi wa habari kutembelea ushoroba huo kupitia Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mwenyekiti wa CCM, Mohamed Msuya amesema vitendo vya tembo kuharibu mazao na watu vimekuwa vikiibua malalamiko kwa wananchi na kuonekana kuwa chama kimeshindwa kuwasaidia, hivyo STEP wamekuja katika kipindi muafaka.

Msuya amesema chama kipo bega kwa bega na mdau yoyote ambaye anatekeleza malengo yote ambayo yanatajwa ndani ya Ilani ya CCM na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano zaidi.

“Ushoroba wa Kilombero ambao unarejeshwa na STEP una afya ndani ya chama na sisi tutaendelea kuunga mkono yoyote, kwani kadhia ya tembo kwa wakazi wa Sole, Mang’ula A na Kanyenja yalikuwa makubwa na kutumika kama kete ya kisiasa,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema vitendo vya tembo kuingia mashambani vilikuwa vinasababisha hasara kwa wakulima, hivyo ni matumaini yake kuwa kupitia ushoroba huo kadhia hiyo itaisha na uzalishaji utaongezeka.

Amesema mradi huo wa ujenzi wa ushoroba utarudisha imani ya wananchi kwa serikali na tembo watakuwa sehemu ya jamii.

“Sisi tunaipongeza Serikali kwa kukarabisha wadau mbalimbali katika utatuzi wa kero za wananchi, hii inatusaidia sisi wasimamizi kuwa na cha kuzungumza mbele yao. Unajua haingii akilini mtu anauwawa ahalafu analipwa fidia ambayo haiendani na thamani yake, ila hili la kurejesha ushoroba ni la kuungwa mkono,” amesema.

Naye Mkazi wa kijiji cha Mang’ula A, Nicholaus Kasangaya amesema wamefurahi ujemzi wa ushoroba kwa kuwa utawafanya wanavijiji kuwa salama katika maeneo yao.

Kasangaya amesema kupitia ushoroba huo ambao unaunganisha Hifadhi ya Udzungwa na Nyerere utachochea utalii katika wilaya yao, hivyo kuongeza kipato.

“Sisi kama wakazi wa eneo hili tunawapongeza STEP kwa uamuzi wao wa kurejesha ushoroba huu ambao unadaiwa kuwa na historia kubwa katika wilaya yetu,” amesema.

Meneja wa STEP Kilombero, Joseph Mwenegelo amesema hadi sasa zaidi ya wananchi 300 wamelipwa fidia ya takribani bilioni 2 ili kupisha ujenzi wa Ushoroba wa Tembo Kilombero,

Ametaja vijiji vilivyohusika ni mradi huo ni Sole ambapo awamu ya kwanza mashamba 19 yalilipwa fidia ya shilingi milioni 127.6, Kanyenja 147 shilingi milioni 650.6 na Mang’ula A 113 shilingi milioni 942.2 hiyo ikiwa ni jumla ya mashamba 279 yamelipwa shilingi bilioni 1.72.

“Awamu ya pili Sole mashamba manee yamelipwa shilingi milioni 16, Kanyenja 38 shilingi milioni 158.7 na Mang’ula A 10 shilingi milioni 96.7 sawa na mashamba 52 yaliyolipwa shilingi milioni 271.5,” amesema.

Mwalugelo amesema STEP kwa kushirikiana na wadau wengine wamepima eneo lenye kilomita za mraba 12.5 ambapo kijiji cha Kanyenja kimechukuliwa asilimia 5, Mang’ula A asilimia 11 na Sole asilimia 7.

Post a Comment

0 Comments