Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WATENDAJI WA SERIKALI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali wasiwe kikwazo waendelee kutoa ushirikiano viongozi wa dini na wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji na kushirikiana na sekta binafsi pamoja na madhehebu yote ya dini katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

“Katika hili nasisitiza watendaji wote wa Serikali kuendelea kuziunga mkono taasisi binafsi zinazotoa huduma kwa wananchi ili ziweze kutimiza malengo yake.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 20, 2023) katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini Arusha.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Askofu Mkuu wa Makanisa ya International Evangelism na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Eliud Issangya kwa kuongoza vema chuo hiko ambacho kimetimiza miaka 40.

“Nimefurahi sana kusikia idadi ya wahitimu wa chuo hiki imefikia zaidi ya 10,000 ama kwa hakika mmeweza kuweka hazina kubwa ya watendaji katika shamba la Mungu.”

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinakikabili chuo hicho ikiwemo ya barabara, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TARURA mkoani Arusha kuhakikisha barabara hiyo ya kutoka Kikatiti hadi Sakila inakarabatiwa.

Naye, Dkt. Issangya amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha maridhiano na kuwatua moyo viongozi wa dini, hivyo kuwawezesha kutekeleaza majukumu yao kwa urahisi.

Amesema uimara wa Serikali umewawezesha viongozi wa dini zote nchini kupendana, kufanya kazi kwa kushirikiana, kuaminiana na kuheshimiana.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la International Evangelism la nchini Congo, Askofu Byamungu Magala ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu.

“Tanzania ni Taifa ambalo limejaa amani na utulivu na ni Taifa ambalo halina ubaguzi wa dini wala kabila, Taifa zuri linalopokea wageni bila ya shida yoyote. Nawapongeza viongozi wa Taifa hili.”

Amesema nchini kwao kuna matatizo hawana utulivu, hivyo hawawezezi kumuamudu Mwenyezi Mungu kwa amani kama ilivyo Tanzania.

“Kila ninapokuja hapa namuomba Mungu nasi atupe amani. Amani hii mliyonayo mnatakiwa kuilinda kwa sababu Taifa bila amani raia watakuwa na matatizo makubwa, sisi watu wanauawa kinyama.”

Pia, amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri na kumtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhudhuria sherehe hizo. “Hali hii inaonesha namna ambavyo viongozi wa Serikali wako karibu na raia na wanyenyekevu sana tofauti na kwetu.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhmisho ya Miaka 40 ya Chuo cha Biblia Sakila kilichopo Arumeru mkoani Arusha, Juni 20, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)




Baadhi ya Washiriki wa Maadhimisho ya Miaka 40 ya Chuo cha Biblia Sakila kilichopo Arumeru mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza Juni 20, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia maelefu ya washiriki wa Maadhimisho ya Miaka 40 ya Chuo cha Biblia Sakila kilichopo Arumeru mkoani Arusha, Juni 20, 2023. Kushoto kwake ni Muasisi wa Chuo hicho, Askofu Dkt. Eliud Issangya na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha wageni wakati alipowasili kwenye Ofisi Kuu ya Chuo cha Biblia Sakila kuongoza Maadhimisho ya Miaka 40 ya Chuo hicho kilichopo Arumeru mkoani Arusha, Juni 20, 2023. Katikati ni Muasisi wa Chuo hicho, Askofu Dkt. Eliud Issangya na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments