SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari sasa inaendesha zoezi la uhakiki wa taarifa za anuani za makazi ili kwa wale ambao waliachwa na mchakato wa awamu ya kwanza waweze kupatiwa anuani sambamba na kuhakikiwa taarifa zao.
Zoezi hilo linatarajiwa kuanza katika wilaya ya Ubungo kabla halijasambaa kwenye wilaya nyingine ni jukumu la wakuu wa wilaya, madiwani, wakurugenzi na wenye viti wa serikali za mitaa kuwahamasisha wananchi wote wa ubungo kuhakikisha wanatumia vyema nafasi hii kuwa wanafahamu anuani za makazi yao na kuwa zimesajiwa vyema ambao ndio mfumo wa msingi wa utambuzi nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Juni 28, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Albert Chalamila amewataka wakazi wa wilaya ya ubungo kupitia zoezi hili kuhakikisha wanajua namba ya nyumba anayoishi, jina la barabara yake na postcode ya kata yake ili kurahisisha kufikiwa na huduma kwa urahisi.
Mheshimiwa Chalamila ameziomba taasisi za dini kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha zoezi hili, wananchi waendelee kujiwekea miundombinu ya mfumo wa anuani za makazi yao yaani kuweka vibao vyenye namba za nyumba zao na nguzo za majina ya barabara ili manispaa ya ubungo kuwa na mfumo wake.
“Watendaji wa kata Pamoja na wa mitaa na wadau wengine wote mnawajibu wa kusimamia vyema zoezi hili katika maeneo yenu, pia wananchi wanapaswa kufahamu kwamba kibao cha namba, nyumba ndani ya mkoa wa Dar es Salaam hakitakiwi kuzidi shilingi elfu 5, sitamfumbia macho yeyote atakayefanya udanganyifu kupitia zoezi hili la anuani za makazi” amesema Chalamila
Hivyo, Chalamila amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analiendesha zoezi hili kwa watanzania wote, mchakato huu unatumia fedha nyingi kwa mantiki hiyo watanzania na hasa wanaubungo waweze kujitikeza vizuri pale wanapopata elimu hii ili wizara iweze kufanya kazi yake kwa ukamilifu.
0 Comments