**********
Wananchi wa Mtaa wa Mayeto-Hombolo Makulu,Jijini Dodoma wamemshukuru Mh. Rais Dr Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa ujenzi wa Shule ya Msingi Mpya ya Mayeto ambayo itasaidia kupunguza mwendo wa Kilomita 12 walizokuwa wakizitumia kila siku kutembea kwenda katika shule za mitaa ya Jirani.
Wananchi hao wametoa shukrani zao jana kupitia Diwani wa Kata ya Hombolo Makulu Mh. Gideon Nkana wakati wa wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde alipokuwa akipita kutembelea na kukagua hatua za ujenzi wa shule hiyo.
“Kwa niaba ya wananchi wangu hawa wote,ninamshukuru sana Mh Rais kwa ujenzi wa shule hii ambao utasaidia sana kuwapunguzia mwendo watoto wa shule ambao awali walikuwa wanakwenda umbali mrefu kufuata huduma hii.Ninataka kuwahakikishia Rais wangu na Mbunge wangu kwamba wananchi wa Mayeto tupo nao bega kwa bega katika kushirikiana nao kuleta maendeleo”Alisema Diwani
Naye Afisa Elimu Msingi Jiji la Dodoma Bi. Prisca Myalla amesema ujenzi wa madarasa 9 na matundu ya vyoo 10 chini ya mradi wa BOOST unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni,2023 ili ifikapo Julai 2023 wanafunzi waanze kuyatumia madarasa hayo.
Akizungumza na wananchi hao,Mbunge Mavunde amemshukuru Mh Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu wa ujenzi wa Shule na kuwataka wananchi kuitunza na kuiendeleza shule hiyo.
“Mtakumbuka miaka 6 iliyopita mimi na ninyi tulichimba msingi na kuanza ujenzi wa Shule hii ya Msingi ya Mayeto.
Ninamshukuru Mh Rais kupitia mradi wa BOOST jumla ya Tsh 318,000,000 zimeletwa hapa kukamilisha ndoto yetu ya miaka mingi sambamba na ujenzi wa Sekondari uliokamilika ndani ya eneo hili ambao umetumia zaidi ya Tsh 400,000,000
Ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunatunza miundombinu ya Shule hii, na pia kusisitiza watoto wetu kutumia nafasi hii kujielimisha ili kuja kuwa msaada kwa jamii yetu.
Mimi kwa nafasi yangu nitawaunganishia umeme hapa shuleni na pia nitawanunulia Computer kwa ajili ya shughuli za shule”Alisema Mavunde
0 Comments