Ticker

    Loading......

WAHARIRI WAPEWA MAFUNZO YA SHERIA NA KANUNI ZA ULINZI KWA WATOA TAARIFA NA MASHAHIDI

Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria bwana Khalist Luanda ambaye ndiye mwezeshaji wa mafunzo haya akitoa wasilisho kwa wahariri na wanahabari wandamizi walioshiriki mafunzo hayo 24/06/2023Sehemu ya wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari na watumishi kutoka Wizara ya katiba na Sheria wakifuatilia mafunzo mjini Singida.Jesse Kwayu Mhariri mwandamizi akiuliza swali katika kikao cha mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria na Jukwaa la wahariri Singida leo 24/06/2023Mhariri kutoka FAMA bwana Neville Meena akichangia jambo katika mafunzo kwa wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya Sheria ya kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Ulinzi wa Mashahidi.Sehemu ya wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari na watumishi kutoka Wizara ya katiba na Sheria wakiendelea na mafunzo mjini Singida.

**************

Na Lusajo Mwakabuku,JamhuriMedia,Singida

Wizara ya Katiba na Sheria imeendesha mafunzo kwa wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya Sheria ya kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Ulinzi wa Mashahidi, Sura ya 446 (The Whistleblower and Witness Protection Act, Cap 446) kwa lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.

Mafunzo haya kwa wanahabari yamefanyika Juni 24, 2023 mkoani Singida yakijumuisha wanahabari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwa madhumuni ya kuwajengea uelewa wa sheria na kanuni hizi nyeti kwa kina ili waweze kuzifafanua na kuzisambaza kwa Watanzania wote kupitia habari zitakazoletwa na waandishi wa vyombo vyao vya habari.

Akiifafanua sheria hiyo wakati akifanya wasilisho mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Khalist Luanda, amesema sheria inalenga kuhimiza na kuwezesha utoaji taarifa za makosa ya kupanga, makosa ya rushwa, mienendo isiyo ya maadili, matumizi mabaya ya ofisi, matendo hatarishi na ya ukiukaji wa sheria.

Aidha Luanda ameongeza kuwa sheria hii pia inalenga kutoa ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi dhidi ya matendo ya kulipiza kisasi na kuweka mfumo wa kutoa zawadi na fidia kwa watoa taarifa na mashahidi ambao taarifa zao zitasaidia kukomeshwa ama kuzuiwa kwa matukio ya uhalifu.

Luanda amewaeleza wahariri masuala mbalimbali ya uhalifu ambayo mtu anaweza kutoa taarifa kwa maslahi ya Umma na sehemu ambazo mtoa taarifa anaweza kutoa taarifa ikiwa ni pamoja na kwa mwenyekiti au mjumbe wa Serikali ya kijiji,kiongozi wa taasisi ya dini, diwani, meya au mwenyekiti wa halmashauri au mbunge na kuwa viongozi hao wanatakiwa kutunza siri za taarifa walizopatiwa na mtoa taarifa.

Katika suala la ulinzi wa mashahidi amewaeleza wanahabari hao ikiwa mamlaka au kwa maombi ya shahidi au kutokana na taarifa ilizozipata, inaona shahidi anaweza kufukuzwa au kusimamishwa kazi, kunyanyaswa, kubaguliwa, kutishwa na mwajiri,maisha yake au mali zake, maisha au mali za mtu wake wa karibu ziko hatarini au kuna uwezekano wa kuwa hatarini basi mamlaka itawasilisha suala hilo kwenye Taasisi yenye uwezo wa kumlinda shahidi.

Katika kuwalinda, mamlaka inaweza kuchukua hatua ya kumhamisha shahidi kituo cha kazi au makazi na pia kwa madhumuni ya kuchochea hamasa ya kutoa taarifa, mtoa taarifa au shahidi anaweza kupewa zawadi au fidia kwa utaratibu uliowekwa na Kanuni.

Katika kuhakikisha usalama wa mtoa taarifa unazingatiwa, amesema mamlaka au mtu yoyote anayefanya kazi za mamlaka ambaye atatoa siri kuhusu utambulisho wa mtoa taarifa atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka mitano au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni 15 au vyote kwa pamoja.

Lakini pia mamlaka ambayo itashindwa kuchukua hatua kuhusu taarifa iliyotolewa na kushindwa huko kumesababisha hasara kwa taasisi ya umma, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka mitano au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni 15 au vyote kwa pamoja.

Lakini pia Sheria hii pia inamuwajibisha mtoa taarifa ambaye kwa makusudi atatoa taarifa za uongo zinazohusu uhalifu, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni 3 au vyote kwa pamoja.

Pia ikiwa mtoa taarifa atatoa siri za mtu ambaye taarifa za uhalifu zimetolewa dhidi yake, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atahukumiwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni 3 au vyote kwa pamoja.

Mwaka, 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria hii ya kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Ulinzi wa Mashahidi. Wizara ya Katiba na Sheria imepewa dhamana ya kusimamia Sheria hii ambayo imempa Waziri wa Katiba na Sheria mamlaka ya kutengeneza Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi kwenye kifungu cha 15 cha Sura ya 446.

Aidha,wizara katika kuhakikisha Sheria inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia madhumuni ya sheria, kupitia mradi wa BSAAT ilikamilisha kutunga Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi (The Whistleblower and Witness Protection Regulations) na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Namba 59 la tarehe 10 Februari, 2023. Madhumuni ya kanuni hizi ni kutoa ulinzi, motisha na kulipa fidia kwa watoa taarifa za uhalifu na mashahidi, ili kuwaongezea imani na kuimarisha usalama wao.

Post a Comment

0 Comments