Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS KANDA YA MAGHARIBI YAFANYA MSAKO DUKA KWA DUKA

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi limeendesha operesheni maalum ya kutoa elimu na kukagua bidhaa zilizopigwa marufuku kutumika nchini.
Bidhaa hizo ni mafuta ya magari aina ya dot 3, nyaya za umeme na nguo za ndani za mitumba.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusiana na operesheni hiyo, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Rodney Alananga ,alisema operesheni hiyo ilianza Juni 20, mwaka huu kwenye mikoa hiyo mitatu.

Alisema operesheni hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya viwango. Akianza na nguo za ndani za mitumba, alisema waliweza kukamata tani moja na nusu.

Alisema nguo za ndani za mitumba zinagusana na ngozi na huko zilizotoka zinakuwa zimeishavaliwa, hivyo hauwezi kujua mtumiaji alikuwa na magonjwa gani.

"Hizi nguo za ndani za mitumba zinaweza kuleta magonjwa ya ngozi, tulishatoa elimu kwa wauzaji na waingizaji wa nguo za mitumba, kwamba nguo za ndani hazitakiwi kutumika nchini," alisema Alananga.

Alisema kwa sasa wameamua kushuka na kwenda kutoa elimu hiyo chini kabisa kwa wananchi kuhusiana na madhara ya nguo za ndani za mitumba na kuziondoa sokoni.

Alisema changamoto ni wafanyabiashara ambao sio waaminifu ambao wanazipitisha kwenye njia za panya, kwani wangezipitisha njia halali zingekamatwa kabla ya kuingia nchi na kuzirudisha zilikotoka.

Kuhusu mafuta ya magari aina ya dot 3 alisema yalishapigwa marufuku kutumika nchini kutokana na kutokidhi viwango. Alisema mafuta hayo yanapotumika kwenye magari yanaweza kusababisha moto au breki kufeli na kusababisha uhalibifu wa mali na hata vifo.

Kwa upande wa nyaya za umeme, Alananga alisema zilizokamatwa zilishakatazwa kwenye soko la Tanzania kwa sababu zinaweza kuunguza vitu na hata nyumba.

Alisema bidhaa kutokana nma bidhaa hizo tatu kupigwa marufuku kutumika katika soko la Tanzania, TBS wameendelea kuzifuatilia na ili kuziondoa.

Alisema kwenye operesheni hiyo walikagua wadau 651 na watu 154 walikutwa makosa ya kuuza bidhaa hizo ambapo wamepewa siku 14 za kueleza ni wapi walizinunua hizo bidhaa.

Baada ya hapo alisema watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria, lakini pia watatakiwa kulipia gharama za kuteketeza bidhaa hizo.

Alananga aliwataka Watanzania na watumiaji wazingatia elimu ambayo imekuwa ikitolewa na TBS na wanapoenda kununua bidhaa ni vema wakapata maelekezo kutoka kwa wale wanaowauzia bidhaa husika.

Aidha, alisema wanaponunua bidhaa ni vyema wakapewa nyaraka za hizo bidhaa ili iwe rahisi kufuatilia walioingiza bidhaa.

Post a Comment

0 Comments