Ticker

6/recent/ticker-posts

SIO SIRI DCEA 'UPELE' UMEPATA MKUNAJI MAPAMBANO DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SIO siri mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya nchini Tanzania imeshika kasi.Ndio sote ni mashahidi.

Operesheni mbalimbali za kuwasaka wauza unga ,a.k.a ngada, a.k.a sembe , utamu na aina nyingine yenye maneno mbalimbali imeendelea kufanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya( DCEA).

Tunafahamu operesheni iliyofanywa na Mamlaka hiyo kuanzia Machi 25 mwaka huu hadi Juni imeonesha ni kwa namna gani kazi kubwa inafanywa katika kukomesha dawa za kulevya, kupitia operesheni hiyo dawa za kulevya za aina mbalimbali zimekamatwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro n Arusha.

Ndio hivyo , wamekamatwa na watu kadhaa kutokana na kujihusisha na biashara hiyo , miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na baadhi ya wanawake wa kitanzania ambao wanatumiwa na raia wa kigeni.

Kutoka nchi gani, hiyo inabaki siri ya kambi, sipo tayari kuharibu ushahidi.Ila ujue tu raia wa kigeni wanarubuni dada zetu kwa kuanzisha mahusiano na mwisho wa siku wanajikuta wakiingizwa kwenye biashara hiyo.

Ni mbinu mpya kwa mujibu wa Mamlaka hiyo na tayari wameibaini, baadhi ya wanawake hao jua na mbaramwezi wanaviona kupitia madirisha ya kaselo kadogo.Imekula kwao na ikibainika kwa aina yoyote ile wanahusika wajue jela inawahusu. kwani kuna ubaya gani?

Wanaharibu vijana wa Kitanzania , tunapoteza nguvu kazi ya Taifa, kwanini wanaojihusisha na biashara hiyo waachwe? Tumechoka kuishi na mateja mtaani, tunataka Taifa lenye nguvu kazi yenye nguvu za kutosha kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu.



Huo ndio ukweli na inapotokea mtu anaharibu nguvu kazi hiyo kwa kuilisha dawa za kulevya hatuwezi kukaa kimya.Kamata weka ndani.Ndio habari ya sasa.

Nikiri Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya chini ya uongozi mahiri wa Kamishina Jenerali Aretas Lyimo inafanya kazi kubwa na nzuri katika kukomesha biashara ya dawa za kulevya.

Kasi ya Kamishina Jenerali Lyimo pamoja na timu zima ya watumishi wa Mamlaka hiyo ni kama vile Upele umepata mkunaji, wanapambana usiku na mchana kuhakikisha biashara dawa za kulevya nchini kwetu inakoma, na hakika inawezekana.Ni jukumu la Watanzania wote kushiriki kikamlifu katika vita hiyo, tukiamua tunaweza.

Hata hivyo pamoja na mapambano hayo taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini inaeleza Tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuongezeka nchini na duniani kwa ujumla lakini Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Jemedari wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupambana na tatizo hilo.

Mapambano hayo yanaendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kufuata miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ambayo imeandaliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaeleza bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayolimwa na kutumiwa kwa wingi nchini katika mwaka 2022.

Hekari 179 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na tani 20.58 za dawa hiyo zilikamatwa katika mwaka 2022.Aidha, hivi karibuni imeelezwa kumeibuka tabia ya kuchanganya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi kwenye vyakula kama vile biskuti, asali, juisi, majani ya chai na keki.



Tukiangalia Taarifa ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2022 utaona kuwa asilimia 40 ya nchi za wenzetu waliohalalisha matumizi ya bangi, zilikumbwa na idadi kubwa ya magonjwa ya afya ya akili yaliyosababishwa na matumizi ya dawa hiyo.

Hali hiyo inalifanya Taifa letu liendelee kuharamisha bangi ili kuwakinga vijana wetu. Operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, zilifanikisha kukamata tani 15.2 za mirungi, kilo 254. 7 za heroin na kilo 1.7 ya cocaine.

Aidha, kumekuwa na mwendelezo wa ukamataji wa dawa ya kulevya aina ya methamphertamine ambapo kwa mara ya kwanza zilikamatwa mwaka 2021 kiasi cha kilo 430.8 na kufuatiwa na mwaka 2022 ambapo gramu 968.7 zilikamatwa.

Vilevile, mwaka 2022 umeshuhudia ukamataji wa dawa nyingine ngeni nchini inayojulikana kama mescaline ambapo gramu 56 zilikamatwa.

Kwa mara ya kwanza nchini, Serikali imefanikiwa kuandaa “Mwongozo wa Utoaji Elimu Juu ya Tatizo la Dawa za Kulevya Nchini” ili kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi juu ya tatizo hili.

Jitihada za kujengea uwezo walimu wa walimu zimeanza na tayari wahitimu kutoka asasi 27 za Mkoa wa Dar es Salaam wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa makundi mengine.Serikali imeendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha elimu dhidi ya tatizo la dawa za kulevya inatolewa kwenye jamii.

Kuhusu tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya iliendelea kutolewa ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya waraibu 871,010 walinufaika na tiba hiyo nchini. Aidha, Serikali imeendelea kufadhili mafunzo ya stadi za kazi kwa waraibu wanaopata nafuu ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Mafanikio hayo ni matunda ya ushirikiano mkubwa baina ya wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla. Nawapongeza kwa jitihada hizi.

Katika taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini , Jenista Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ametumia nafasi hiyo kuhimiza kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu katika kuhakikisha anatoa taarifa ya wanaojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya na kuwasaidia wale waliopata uraibu kupata tiba.

Akiizungumzia kwa kina Kamishina Jenerali Lyimo anasema wameandaa taarifa hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Na 5 ya Mwaka 2015, ambacho kinailekeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya kuandaa na kuiwasilisha Bungeni.

Anasema lengo la taarifa ni kuitaarifu jamii kuhusu hali ya tatizo la dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022 pamoja na jitihada zilizofanyika katika kukabiliana nalo huku akitaja nguzo muhimu nne zinazotumika kupambana na tatizo la dawa za kulevya Nchini na mikakati yake.

Nguzo hizo ni Kupunguza Upatikanaji wa Dawa za Kulevya, Kupunguza Uhitaji wa Dawa za Kulevya, Kupunguza Madhara ya Matumizi ya Dawa za Kulevya na
Kuimarisha Ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Aidha katika taarifa hiyo inatoa changamoto zilizojitokeza katika udhibiti wa dawa za kulevya nchini na mikakati yake.Kwakuwa tatizo la dawa za kulevya ni mtambuka, linahitaji juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo.

"Natoa shukrani za pekee kwa wadau wote walioshiriki katika mapambano haya na kuwasilisha taarifa zao. Tuendeleze umoja wetu ili kuishinda vita hii na kufikia lengo la kuwa na Tanzania isiyojihusisha na dawa za kulevya, " anasema Kamishina Jenerali Lyimo alipokuwa akiielezea taarifa hiyo.

VIPI KUHUSU HALI YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI?

Kwa mujibu wa Kamishina Jenerali Lyimo anasema taarifa ya hali ya dawa za kulevya duniani ya mwaka 2022 ilionesha matumizi ya dawa za kulevya yaliendelea kuongezeka duniani.

Kulingana na taarifa hiyo inakadiriwa kuwa takribani watu milioni 284 wenye miaka kati ya 15 hadi 64 walitumia dawa za kulevya duniani mwaka 2020. Idadi hii ni inafanya ongezeko la asilimia 26 toka mwaka 2010 ambapo ilikadiriwa kuwa watu waliotumia dawa za kulevya walikuwa milioni 226.

Katika kipindi hicho, dawa za kulevya aina ya bangi, heroin, metamphetamine, cocaine pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya zilitumika zaidi. Katika kipindi hicho kulishuhudiwa ongezeko kubwa la uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa mpya za kulevya (New Psychotropic Substances-NPS) kuwahi kutokea duniani.

"Matumizi ya dawa za kulevya yaliripotiwa kusababisha madhara
ya kiafya kwa watumiaji na jamii, kama vile ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI, magonjwa ya afya ya akili na homa ya ini. Hata hivyo jitihada mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa, " anasema.

VIPI KUHUSU BANGI

Taarifa ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2022, ilionesha bangi
imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayotumiwa zaidi duniani. Takribani watu milioni 209 walitumia bangi mwaka 2020, ikiwa ni sawa na asilimia nne (4) ya watu duniani kote, huku idadi ya watu wanaotumia bangi ikiongezeka kwa asilimia 23 katika muongo mmoja uliopita.

Matumizi ya bangi yameendelea kuwa ya juu zaidi Amerika Kaskazini, ambapo asilimia 16.6 ya wakazi wanatumia dawa hiyo, huku ikiendelea kuwa dawa inayosumbua watu wengi wanaotibiwa barani Afrika.

Pia taarifa hiyo ilionesha kuwa mwaka 2020, kilimo na ukamataji wa bangi duniani uliongezeka hadi kufikia rekodi ya juu zaidi.Aidha, asilimia 40 ya nchi zilionesha kuwa idadi kubwa ya magonjwa ya afya ya akili yalisababishwa na matumizi ya bangi.

Wakati asilimia 33 zilionesha bangi kama dawa inayowasumbua zaidi hususani wale walio kwenye tiba za uraibu wa dawa za kulevya.Idadi kubwa zaidi ya watu wanaopatiwa tiba ya uraibu wa dawa za kulevya barani Afrika na baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini na Caribbean, ni wale wanaotafuta usaidizi wa matatizo ya afya ya akili yanayosababishwa na matumizi
ya bangi.


UHALALISHAJI WA BANGI NA ATHARI ZAKE

Taarifa ya Dawa za Kulevya Duniani 2022 ina viashiria vya awali vinavyoonesha
kuwa uhalalishaji wa bangi katika maeneo ya Amerika Kaskazini na maeneo mengine umeleta athari kubwa hususani kwa afya ya jamii, usalama, mabadiliko ya masoko, ongezeko la biashara nyingine haramu (Usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya silaha za magendo) na kuathiri mapambano dhidi ya uhalifu.

Bidhaa za bangi zimetofautiana ambapo viwango vya wastani vya kemikali inayosababisha uraibu kwenye bangi inayoitwa Tetrahydrocannabinol (THC) katika bidhaa mbalimbali za bangi kama biskuti na keki vimeendelea kuongezeka kufikia asilimia 60 kutoka kiwango cha asilimia tano (5) cha kemikali hiyo.

"Taarifa kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (United Nations Office on Drugs and Crime-UNODC) ilionesha kuwa mitazamo hasi juu ya madhara ya bangi imeendelea kupungua katika maeneo yaliyohalalisha matumizi ya dawa hizo, " anasema Kamishina Jenerali Lyimo kwenye taarifa hiyo.

Wakati huo huo, kumekua na ongezeko la watu walio na magonjwa ya afya ya akili na watu wanaojiua kutokana na matumizi ya bangi, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu waliolazwa hospitalini kwa kuzidisha kiwango cha matumizi.

Kuhusu Dawa za Kulevya Jamii ya Afyuni ni kwamba dawa hizo zipo katika kundi la vipumbaza na hutengezwa kutokana na mmea wa afyuni (opium poppy) kwa kuchakatwa na kemikali bashirifu, na hivyo kuzalisha dawa za kulevya aina ya heroin na morphine (opiates).

Kwa mujibu wa Taarifa ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2022, ilikadiriwa kuwa watu milioni 61 walitumia dawa za kulevya jamii ya afyuni mwaka 2020, ikiwa ni asilimia 1.2
ya idadi ya watu duniani.

Takribani asilimia 40 ya waraibu waliokuwa kwenye tiba waliathiriwa zaidi na dawa za kulevya jamii ya afyuni, iliyosababisha theluthi mbili ya vifo vinavyohusiana moja kwa moja na kuzidisha matumizi ya dawa hiyo
(overdoses).Asilimia 86 ya uzalishaji haramu wa afyuni duniani umetokea nchini Afghanistan.

Hata hivyo iliripotiwa kuwa njia ya Balkan ambayo huanzia nchi Afghanistan, Iran,
Uturuki hadi Nchi za Ulaya imeendelea kuwa njia kuu ya usafirishaji wa dawa za
kulevya jamii ya afyuni, huku ukamataji wa dawa zinazosafirishwa na watu binafsi ukiongezeka kwa mwaka 2021.


VIPI KUHUSU COCAINE?

Kwa mujibu wa Taarifa ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2022, ilikadiriwa kuwa watu milioni 21.5 walitumia cocaine mwaka 2020, ikiwa ni sawa na asilimia 0.4 ya idadi ya watu duniani.

Katika taarifa hiyo ilionesha kuwa Amerika Kaskazini na Ulaya zimendelea kuwa masoko makuu ya biashara ya cocaine. Hata hivyo, iliripotiwa kuwa uhitaji wa dawa hiyo katika bara la Afrika na Asia umeongezeka maradufu katika miongo miwili iliyopita.

Kiwango cha uzalishaji wa cocaine kilifikia rekodi ya juu zaidi mnamo mwaka 2020, ikifikia takribani tani 1,982, wakati ukamataji uliongezeka zaidi karibu na maeneo ya uzalishaji.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2022, inaonesha kuwa biashara na usafirishaji wa cocaine kwa njia ya bahari unazidi kushika kasi na karibu asilimia 90 ya kiasi cha cocaine kilichokamatwa kilihusishwa na shughuli za kiuchumi zinazofanyika baharini.

Kiasi kikubwa cha cocaine huzalishwa
na husafirishwa kutoka Amerika Kusini hadi Ulaya kupitia Afrika Magharibi
na Kaskazini. Hata hivyo, soko la cocaine limeongezeka zaidi nje ya maeneo
yaliyozoeleka kwa biashara hiyo (Amerika Kaskazini, Ulaya Magharibi, Afrika na
Asia).

Hata hivyo kwa leo itoshe , tuishie hapo na siku zijazo Michuzi Blog na Michuzi TV itafafanua kuhusu taarifa hiyo ya hali ya dawa za kulevya na nitumie nafasi hii kukumbusha kuanzia Juni 23 hadi Juni 26 Tanzania itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimaifa duniani kupamba na dawa za kulevya.

Kwa hapa Tanzania maadhimisho hayo yayafanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu atakuwa mgeni rasmi.

Post a Comment

0 Comments