Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIKABIDHI OSHA MAGARI NA VIFAA VYA BILIONI 4.3

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako ameukabidhi Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) magari 13 na vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 2 ambavyo vimetolewa na serikali ili kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo.
Magari na vifaa hivyo vyenye thamani ya jumla ya zaidi ya bilioni 4 vimekabidhiwa leo (Juni 30, 2023) katika hafla maalum iliyofanyika katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na menejimenti na watumishi wa OSHA.

Aidha, hafla hiyo ilienda sambamba na ufunguzi wa mafunzo kwa watumishi wapya 18 ambao wameajiriwa ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuboresha utendaji wa OSHA.

Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Prof. Ndalichako amesema magari na vifaa hivyo vimenunuliwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro ambapo alieleza kuwa serikali yake imepanga kuiongezea hadhi Taasisi ya OSHA.

“Haya yote yanafanyika leo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) 2023 yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro. Mheshimiwa Rais aliahidi kununua magari 13 na kuajiri watumishi wapya 18 ili kuiongezea Taasisi ya OSHA uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yake,” ameeleza Waziri Ndalichako na kuongeza:

“Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) napenda kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Rais wetu Mama Samia kwa kutambua umuhimu wa Taasisi ya OSHA hapa nchini na kuamua kwa dhati kuipandisha hadhi na kuipa uwezo zaidi wa kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda nguvukazi ya Taifa hili pamoja na mitaji ya wawekezaji kwa kuwezesha upatikanaji wa vyombo hivi muhimu vya usafiri, vifaa vya kaguzi pamoja na kuongeza idadi ya watumishi.”

Kwa mujibu wa Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, uwezeshaji huo wa serikali kwa OSHA utaongeza kasi na hamasi katika kukamilisha mchakato wa nchi kuridhia Mikataba ya Kimataifa Na. 155 na 187 kuhusu masuala ya usalama na afya kazini pamoja na kufanikisha utekelezaji wa sera ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuinua sekta ya biashara na uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema magari na vifaa vya ukaguzi walivyokabidhiwa vitarahisisha kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya OSHA hususan kaguzi kwenye maeneo ya kazi pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi.

Aidha, ameiomba serikali kuendelea kuijengea uwezo Taasisi ya OSHA kutokana na uzito wa majukumu iliyonayo ya kusimamia usalama na afya katika maeneo yote ya kazi nchini.

“Hivyo, kwa niaba ya Menejimenti nzima ya OSHA, nirudie tena kukushukuru sana wewe binafsi na Ofisi nzima ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwa miongozo yenu ya kila mara na tunaomba utufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake ya kutupatia watumishi pamoja na magari mapya”, ameeleza Kiongozi Mkuu wa OSHA Bi. Mwenda.
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na watumishi wa OSHA mapema baada ya kuwasili katika ofisi za OSHA Dar es Salaam kwaajili ya hafla za kukabidhi magari 13 pamoja na kuwakaribisha watumishi wapya 18 katika taasisi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akizungumza na watumishi wa OSHA mbele ya Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako (hayuko pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi magari 13 pamoja na kuwakaribisha watumishi wapya 18 iliyofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Menejimenti ya OSHA pamoja na watumishi wa Taasisi hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi magari 13 pamoja na kuwakaribisha watumishi wapya 18 katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi wa OSHA wakifuatilia hotuba za Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda pamoja na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako (hawapo pichani).

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akikata utepe kama ishara ya kuzindua na kukabidhi magari 13 kwa taasisi ya OSHA. Kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA, Bi. Netiwe Mhando.

Watumishi wapya wa OSHA wakifuatilia hotuba za Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda pamoja na Waziri wa Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako (hawapo pichani).
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda, wakikabidhi sanduku la vifaa vya ukaguzi kwa watumishi wa OSHA.Vifaa hivyo ni kati ya vifaa vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 2 vilivyotolewa na serikali kwa OSHA ili kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo.

Post a Comment

0 Comments