Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA SOUTH BRIDGE



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 08 Juni 2023 amefanya mazungumzo na wawakilishi wa Taasisi ya South-Bridge wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji Dkt. Frannie Leautier ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao, Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 08 Juni 2023.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Makamu wa Rais ameikaribisha taasisi hiyo kuiunga mkono Tanzania na kusaidia kutafuta rasilimali fedha kwaajili ya miradi mbalimbali ya kimkakati kama vile Nishati, Kilimo, Mazingira na Miundombinu. Pia ameikaribisha taasisi hiyo kushiriki katika kuendeleza miradi iliopo katika hatua za andiko dhana ili ifikie hatua ya kupata ufadhili wa kifedha.

Pia ameikaribisha Taasisi ya South – Bridge kushiriki katika miradi ya Uchumi wa Buluu Zanzibar kama vile ujenzi wa Bandari nne za Uvuvi katika eneo la Unguja na Pemba, kushiriki katika miradi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ikiwemo eneo la Tabora – Kigoma kilometa 506 na Eneo la Mtwara – Mchuchuma – Liganga Kilometa 1000.

Vilevile Makamu wa Rais ametaja miradi ya ushirikiano na Taasisi hiyo ikiwemo ya kutambua maeneo muhimu ya uwekezaji katika biashara ya kaboni, Miradi ya kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya hatari za mafuriko kwa maisha endelevu na usalama wa chakula katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko nchini Tanzania pamoja na kuimarisha uwezo wa jamii zinazoishi kando ya bahari na maziwa makuu ili kukabiliana na hatari na athari za kupanda kwa kina cha maji.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ni eneo muhimu kikanda na kidunia kwani ina uwezo mkubwa wa kuwa na upatikanaji wa kutosha wa chakula, kitovu cha biashara na chanzo kikuu cha madini muhimu pamoja na utajiri wa viumbe hai.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uwekezaji wa South-Bridge Dkt. Frannie Leautier amesema taasisi hiyo imejikita katika kuunga mkono jitihada za mataifa ya Afrika katika kuimarisha mifumo ya kibenki, kuimarisha teknolojia kutokana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali, kuunga mkono miradi ya mazingira kutoka na hatari ya mabadiliko ya tabianchi Afrika pamoja na kuimarisha uchumi jumuishi unaolenga wanawake na vijana kushiriki katika biashara ndogo na za kati.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Waziri wa Nishati January Makamba, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweri pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na wawakilishi wa Taasisi ya South-Bridge wakiongozwa na Dkt. Frannie Leautier ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao, Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 08 Juni 2023.

Post a Comment

0 Comments