Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV- Dodoma
BAADA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani pamoja na kuangalia uhai wa Chama hicho katika wilaya zote za Mkoa huo , kesho Jumapili anatarajia kuhitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Chongolo aliyekuwa ameambatana na wajumbe wawili wa Sekretarieti ambao ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC-Oganaizesheni Issa Hajji Gavu atahitimisha ziara hiyo katika Jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu alianza ziara yake katika Mkoa wa Dodoma Juni 15 , 2023 na amepita katika Wilaya za Mpwapwa, Kondoa, Chemba, Bahi, Kongwa na Chamwino ambapo mbali ya kukagua utekelezaji wa Ilani amepata nafasi ya kusikiliza changamoto za wananchi.
Changamoto hizo zilikuwa zinatolewa na wananchi katika mikutano ya hadhara na vikao vya Chama vilivyokuwa vinafanyika katika ngazi ya Shina ,na miongoni mwa changamoto alizopokea ni ucheleweshaji wa ulipaji fidia kwa wananchi walioathiriwa na tembo.
Pia katika ziara hiyo Chongolo amesikiliza malalamiko ya kuchelewa kwa kutekelezwa kwa miradi ya skimu za kilimo cha umwagialiji na akiwa Wilaya ya Kondoa alipokea kilio cha uhaba wa chakula hasa jimbo la Kondoa Vijijini kiasi cha kumuomba Katibu Mkuu huyo kufikisha ombi lao kwa Serikali ione uwezekano wa kuwapatia chakula.
Mengine ambayo Chongolo ameyapokea kama changamoto za wananchi ni changamoto ya uhaba wa maji, migogoro ya ardhi , afya na miundombinu.
Hata hivyo kesho atakapokuwa anahitimisha ziara yake Katibu Mkuu amekuwa na utamaduni wa kufanya majumuisho yanayokwenda sambamba na kutoa maelekezo kwa watendaji na viongozi wa ngazi mbalimbali, lengo likiwa kuona changamoto zote zipatiwa ufumbuzi.
Pamoja na mambo mengine Mkutano huo utakaofanyika katika viwanja vya Central Sekondari, Katibu Mkuu atawasikiliza wananchi kwa lengo la kuibua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
0 Comments